Na Mwandishi Wetu
VIONGOZI wanane waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanatarajiwa kupandishwa kizimbani wiki ijayo wakikabiliwa na tuhuma za kudharau na kukaidi amri halali ya mahakama, hatua inayoweka hatarini kupelekwa gerezani kwa kifungo cha hadi miezi sita.
Taarifa za uhakika zinasema kesi hiyo tayari imesajiliwa mahakamani kwa namba 000014659, ikidai kuwa viongozi hao waliendelea kushiriki shughuli za kisiasa hadharani licha ya kuwepo kwa amri ya muda ya mahakama iliyowazuia kufanya hivyo hadi pale uamuzi wa kesi ya msingi utakapotolewa.
Imeelezwa kuwa tangu kutolewa kwa zuio la mahakama, kuwa viongozi hao hawapaswi kufanya shughuli za kisiasa kwa mwamvuli wa chama au kutumia ofisi na mali nyingine za chama, imedaiwa kuwa wamendelea kufanya hivyo kinyume na amri ya mahakama.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, viongozi hao wanaweza kupandishwa kizimbani wakati wowote wiki ijayo kujibu mashtaka ya kudharau amri ya mahakama (contempt of court).
Viongozi wa CHADEMA waliotajwa katika kesi hiyo ni:
John Heche – Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara
Amani Golugwa – Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Tanzania Bara
Godbless Lema – Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA na Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini
John Pambalu
Boniface Jacob – Mwenyekiti wa CHADEMA kanda ya Pwani.
Pamela Maassay – Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA)
Hamad Musa Yusufu – Mwanachama wa CHADEMA
Gervas Lyenda-kada mwandamizi wa CHADEMA na John Mnyika -katibu mkuu wa Chadema.
Walalamikaji na Vyeo vyao vya Zamani
Walalamikaji katika kesi hiyo ni wanachama wa zamani wa CHADEMA waliowahi kushika nyadhifa muhimu ndani ya chama:
Said Issa Mohammed – aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar,Ahmed Rashid Khamisi pamoja na Maulidah Anna Komu.
Walalamikaji wanadai kuwa viongozi hao waliendelea kufanya mikutano ya kisiasa, kutoa matamko na kushiriki shughuli za chama hadharani, hatua inayohusishwa na ukiukwaji wa wazi wa amri ya mahakama iliyowataka kusubiri uamuzi wa kesi ya msingi.
Chanzo cha Kesi
Kesi hiyo inatokana na shauri la msingi lililofunguliwa mahakamani na walalamikaji wakipinga baadhi ya maamuzi na shughuli za kisiasa za viongozi wa chama hususani ukosefu wa usawa kwenye Mgawanyo wa fedha za chama hicho baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Kufuatia shauri hilo, mahakama ilitoa amri ya muda (temporary injunction) ikiwazuia viongozi hao kuendelea na shughuli za kisiasa hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.
Hata hivyo, walalamikaji wanadai kuwa viongozi hao waliendelea na shughuli za kisiasa kinyume na zuio la mahakama, jambo lililosababisha kufunguliwa kwa shauri jipya la kudharau amri ya mahakama.
Hatari ya Adhabu
Wataalamu wa sheria wanasema kuwa iwapo mahakama itathibitisha ukiukaji huo, viongozi hao wanaweza kukabiliwa na Faini, au
Kifungo cha hadi miezi sita jela.
Kesi hiyo inatarajiwa kuvuta hisia kubwa za kisiasa na kisheria nchini, huku wadau wakisubiri hatua za mahakama zitakazochukuliwa katika siku zijazo.
