SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 9 Mei 2018

T media news

Rouhani: Kujitoa Marekani katika makubaliano ya JCPOA kunadhihirisha namna Washington haiheshimu makubaliano ya kimataifa

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) kuwa Marekani haikuwa ikiheshimu kivyovyote ahadi na majukumu yake na kwamba kujiondoa kwake katika makubaliano hayo ni jambo lililotarajiwa.

Akijibu uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kujitoa katika makubaliano hayo ya nyuklia, Rais Hassan Rouhani jana usiku alibainisha kuwa: Kuanzia sasa makubaliano hayo yatafuatiliwa kwa kushiriikiana Iran na nchi tano ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza pamoja na Ujerumani. Rais Rouhani ameitaja hatua ya Marekani ya kujitoa katika makubaliano hayo ya kimataifa kuwa ni jambo lililokuwa limekwishatabiriwa na kueleza kuwa, na hapa ninamnukuu, "historia ya miaka arubaini ya Mapinduzi ya Kiislamu na hata kabla yake imetuthibitishia kuwa viongozi wa Marekani siku zote wamekuwa wakiamiliana kiuhasama na taifa kubwa la Iran na mataifa mengine katika eneo; na hawajawahi kuchukua hatua kuhusu kuwepo amani na uthabiti  katika eneo hili na ulimwenguni kwa ujumla. 

Pande husika katika utiaji saini wa makubaliano ya JCPOA

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kutotekeleza ahadi zake serikali ya Trump kuhusu makubaliano mbalimbali ya kimataifa na kueleza kuwa: Uamuzi wa Trump kuhusu makubaliano ya JCPOA ni kuanzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya Iran, lakini akasema taifa lililojizatiti la Iran halitaathirika na vita hivyo vya kisaikolojia.  Ameongeza kuwa makubaliano hayo yataendelea kuimarika licha ya Marekani kushindwa kutimiza wajibu wake na kwamba Iran inaweza kusonga mbele katika njia ya amani kwa kushirikiana na washirika wengine, hata hivyo akasema kuwa, Iran itachukua maamuzi mapya kuhusu makubaliano hayo iwapo maslahi yake hayatadhaminiwa.

Rais Donald Trump wa Marekani jana Jumanne alitoa madai kuwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hayajakuwa na natija na kusaini dikri ya kujitoa nchi hiyo katika makubaliano hayo ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 na kuthibitishwa pia na Umoja wa Mataifa. Marekani imechukua hatua hiyo ya upande mmoja ya kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA katika hali ambayo hadi kufikia sasa nchi mbalimbali zimetangaza uungaji mkono wao kwa makubaliano hayo. Muda mfupi baada ya kutangazwa hatua hiyo ya Marekani ya kujitoa ndani ya JCPOA, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni amejitokeza na kutangaza kufurahishwa na hatua hiyo .