Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ali Mohamed Kessy amesema anao ushahidi wa baadhi ya viongozi wakubwa waliomilikishwa miradi ya maji katika Mkoa wa Rukwa namna wanavyomshawishi ili asizungumze kuhusu ubadhirifu uliopo katika miradi hiyo.
Aidha, alisema kutokana na wakandarasi kupewa miradi kimjomba mjomba imesababisha wananchi wa Nkasi kukosa maji na kipindi cha masika huchimba maji kwenye madimbwi kama panya.
Kessy ametoa kauli hiyo jana Mei 8, bungeni jijini Dodoma wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji ambapo pamoja na mambo mengine amesema viongozi hao wanapewa zabuni za miradi hiyo kiujanja ujanja.
“Awamu ya nne mkandarasi alipewa mabilioni ya fedha, miaka kadhaa sasa bwawa halina maji, wizara inaibiwa hela… na viongozi wakubwa ndiyo wenye miradi, kwa ushahidi wananitafuta ili nizungumze nao nawakatalia, eti mbunge nyamaza, ili waibe zaidi?” alisema.
Pamoja na mambo mengine, alisema katika mkoa huo kumejitokeza ujambazi kwa wakandarasi wa miradi ya maji katika baadhi ya vijiji vya Nkasi ambao hata Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe na Naibu wake, Juma Aweso waliona namna serikali inavyoibiwa fedha.
“Mradi wa Kamwala, mkandarasi ameingia mkataba wa Sh bilioni 7.7 wakati uwezo mdogo, anao uwezo wa kutekeleza miradi ya thamani ya Sh 750 lakini akapewa kijomba mjomba.
“Maelezo bodi ya usajili wa wakandarasi yalieleza kuwa mkandarasi huyu hana sifa, Baraza la Madiwani Nkasi lilimkatalia lakini akapewa kimjomba mjomba,” alisema.