Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa nchi yake imejipanga na iko tayari kuishambulia tena Syria kama itarudia kufanya mashambulizi ya silaha za kemikali.
Onyo hilo la Trump limekuja baada ya Marekani, Ufaransa na Uingereza kufanya mashambulizi katika maeneo matatu ya Syria ndani ya saa 12, kwa kufyatua makombora 100.
Marekani na washirika wake hao wanadai kuwa Syria ilifanya mashambulizi ya silaha za kemikali wiki iliyopita katika eneo la Douma na kusababisha vifo vya watu wasio na hatia, kinyume cha sheria za kimataifa.
Urusi ambao ni washirika wa Syria waliwasilisha hoja katika Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa ikitaka kitendo kilichofanywa na Marekani kulaaniwa vikali na umoja huo, ombi ambalo lilipingwa baada ya mjadala wa muda mrefu uliokuwa na maneno makali, kwa mujibu wa ripoti.
Balozi wa Urusi kwa Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia alisoma nukuu ya maneno ya Rais Vladimir Putin kwa kutekeleza mashambulizi hayo bila kuzingatia sheria za umoja wa mataifa na bila kusubiri majibu ya shirika la upelelezi la umoja wa mataifa linaloshughulikia silaha za kemikali la OPCW.
Wajumbe wa OPCW wanatarajia kuzulu eneo la Douma wiki ijayo kufanya uchunguzi wa tuhuma za Syria kutumia silaha za kemikali.
Syria imekana kutumia silaha hizo na kueleza kuwa tukio hilo limefanywa na waasi kwa lengo la kuichonganisha serikali ya Syria na wananchi wake pamoja na jumuiya za umoja wa mataifa. Rais Bashar Al-Assad ameseam kuwa mashambulizi ya Marekani yanazidi kumuimarisha.