Rais mpya wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume aliyechaguliwa kwa kishindo wikendi hii, amesema katika kipindi chake atahakikisha anashughulikia zaidi suala la utawala wa sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, muda mfupi baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo akipokea kijiti kutoka kwa Tundu Lissu, Fatma amesema kuwa moja kati ya suala linalolalamikiwa na wanachama wengi ni watu kushikiliwa mahabusu kwa muda mrefu bila kupelekwa mahakamani.
“Wanachama wetu wametaka tushughulikie suala la watu kushikiliwa kwa miaka mingi bila kupelekwa mahakamani. DPP anasema bado upelelezi haujakamilika. Sasa wanataka watu wasiendelee kushikiliwa kama upelelezi bado haujakamilika au wafikishwe mahakamani,” alisema.
Akizungumzia tathmini yake kwa mtangulizi wake, alisema alifanya kazi nzuri katika kipindi kifupi alichokuwa ofisini lakini pia hata baada ya kupata matatizo makamu wake aliendelea kufanya kazi nzuri pia.
Fatma ameahidi kutumia nafasi hiyo kuhuisha utawala wa sheria nchini na kuepuka baadhi ya viongozi kufanya kazi kwa kufuata matamko kinyume cha matakwa ya katiba.
Mwanasiasa huyo alipigiwa kura 820 akimuacha kwa mbali Ngwilimi aliyemfuatia akipata kura 363, Mwapongo kura 12 na Wasonga akipata kura 6 kati ya kura 1,195 zilizopigwa na kuhesabiwa. Kipindi chake cha urais kitakamilika baada ya mwaka mmoja.