SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 13 Machi 2018

T media news

Sumatra Yafafanua Ujumbe Huu 'Mke Mmoja Analemaza Akili'

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imetoa ufafanuzi kuhusu tiketi ya basi la daladala yenye ujumbe unaohamasisha wanaume kuwa na wanawake wengi, ambayo imezua gumzo kwenye makundi ya mitandao ya kijamii, ikiwamo WhatsApp.

Tiketi hiyo ambayo inaonekana kudaiwa kuwa ni ya daladala inayofanya safari zake kati ya Mbagala Rangi Tatu na Kivukoni jijini Dar es Salaam, ilizagaa katika mitandao ya kijamii ikiwa na ujumbe usemao 'Mke mmoja analemaza akili.'

Sumatra imewataka abiria watakapopewa tiketi hizo watoe taarifa kwenye mamlaka hiyo kwa kuandika barua ya malalamiko pamoja na kuambatanisha tiketi husika.

Meneja Leseni wa Sumatra, Leo Ngowi alitoa ufafanuzi huo alipoulizwa na Nipashe lililotaka kufahamu kanuni za Sumatra zinasemaje kuhusu maandishi hayo ya kwenye tiketi.

"Hakuna adhabu ya moja kwa moja kwa gari lenye tiketi yenye ujumbe usiokuwa na maadili, lakini gari husika linaweza kuadhibiwa kwa kosa la kushindwa kufuata taratibu, sheria za barabarani, pamoja na sheria zinginezo, ambayo faini yake ni Sh. 250,000," alisema Ngowi.

Ngowi alisema kwa mujibu wa kanuni za Sumatra, kifungu namba 33(2) (a) inayohusu mabasi yaendayo nje ya miji, tiketi zao zinapaswa kuwa na jina la abiria na namba ya kiti.

Alisema tiketi inapaswa kuonyesha muda wa kuwasili na kuondoka kituoni, kituo cha kuondokea, pamoja na njia itakayopita na mwisho wa safari.

Alitaja kingine kuwa ni nauli ya safari, sanduku la posta na namba ya leseni, namba ya usajili ya gari husika, tarehe ya kukata tiketi na siku ya kusafiri, namba ya tiketi, namba ya Sumatra na polisi.

Ngowi alisema kwa magari ya mijini, tiketi zinapashwa kuwa na namba ya usajili ya gari, njia ya gari itakayopitia, nauli halisi, tarehe ya kukata tiketi, pamoja na namba ya leseni.