SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 13 Machi 2018

T media news

Serikali, Airtel Zaanza Mazungumzo

MAZUNGUMZO kati ya kamati maalum iliyoundwa na Rais John Magufuli na kampuni ya Bharti Airtel inayomiliki hisa katika kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania yameanza rasmi jana jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Katika mazungumzo hayo, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais ilisema, kamati iliyoundwa na Magufuli inaongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi na timu ya Bharti Airtel inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wake, Mukesh Bhavnani.

"Mazungumzo hayo yana lengo la kufikia makubaliano yatakayokuwa na tija kwa pande zote mbili (Serikali ya Tanzania na Bharti Airtel) na kuimarisha sekta ya mawasiliano nchini Tanzania," ilisema taarifa ya Ikulu.

Kampuni ya Bharti Airtel iliomba kufanyika kwa mazungumzo hayo baada ya kamati iliyofanya uchunguzi kuhusu umiliki wa kampuni ya Airtel Tanzania kuwasilisha ripoti yake kwa Rais, taarifa hiyo ilisema zaidi.

Mapema mwaka huu kamati hiyo ya uchunguzi ilitoa taarifa iliyosema ubinafsishaji wa kampuni ya Airtel uligubikwa na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu.

Januari 11, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango aliwasilisha taarifa ya kamati kwa Rais Magufuli ambaye aliagiza kufanyika kwa uchunguzi huo Desemba 20, mwaka jana.

Dk. Mpango alisema serikali imejiridhisha kuwa ubinafsishaji wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kwenda Celtel, baadaye kuhamishiwa Zain na sasa Airtel ulifanyika kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu.

Kufuatia ukiukwaji huo, Dk. Mpango alisema serikali inayomiliki asilimia 40 ya hisa za Airtel imeamua kufanya mazungumzo na kampuni ya Airtel inayomiliki asilimia 60 ya hisa, ili nchi iweze kupata haki yake.

“Lakini niwaambie Watanzania yale ambayo tumeyaona ni machafu sana, ni mambo ya ovyo kabisa, nchi yetu kwa kifupi tuliingizwa mkenge, ni fedha nyingi zimepotea kwa hiyo sisi katika majadiliano haya lengo letu litakuwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao,” Dk. Mpango alisema siku hiyo.

Na sasa mazungumzo hayo yameanza, kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu.