Serikali imepanga kukusanya na kutumia Sh32.476 trilioni mwaka ujao wa fedha wa 2018/19.
Akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na kiwango cha ukomo wa bajeti kwa mwaka 2018/19, waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema ukomo wa bajeti umezingatia upatikanaji wa mapato.
Dk Mpango amesema katika mwaka huo Serikali imepanga kutumia Sh20.468 trilioni kwenye matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya bajeti yote.
Matumizi hayo amesema yanajumuisha Sh10 trilioni zitakazolipa deni la Taifa na Sh7.369 trilioni mishahara ya watumishi wakati Sh3.094 trilioni zikielekezwa kwenye matumizi mengine.
Dk Mpango amesema Serikali itatumia Sh12 trilioni sawa na asilimia 37 kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kiasi hicho, amesema kinajumuisha Sh9.876 trilioni sawa na asilimia 82.3 kutoka vyanzo vya ndani na Sh2.13 trilioni sawa na asilimia 17.7 kutoka nje.
Jumla ya mapato ya ndani pamoja na makusanyo ya halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh20.894 trilioni ambayo ni sawa asilimia 64 ya bajeti yote.
“Kati ya mapato hayo yatokanayo na kodi yanatarajiwa kuwa Sh18 trilioni sawa na asilimia 13.6 ya Pato la Taifa,” amesema.
Amesema mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufika Sh2.158 trilioni wakati vyanzo vya halmashauri vikikusanya Sh735.6 bilioni.
Mpango amesema vyanzo vingine vinavyotarajiwa kufanikisha utekelezaji wa bajeti hiyo ni misaada na mikopo yenye masharti nafuu kiasi cha Sh2.676 trilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo ambazo ni sawa na asilimia nane ya bajeti hiyo.
Katika mwaka ujao, amesema Serikali inatarajia kukopa Sh5.793 trilioni kutoka soko la ndani ambazo kati ya hizo, Sh4.6 trilioni zitatumika kulipia hati fungani na dhamana za Serikali zinazoiva.
Sh1.193 trilioni zinazozidi kwenye mikopo hiyo ya ndani ambazo ni sawa na asilimia 0.9 ya Pato la Taifa, amesema ndilo deni jipya.
“Ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miundombinu, Serikali inatarajia kukopa Sh3.111 trilioni kutoka soko la nje,” amesema.