WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amewaamuru wamiliki wa viwanda vitano vya kuchakata minofu ya samaki vilivyoko jijini Mwanza kulipa faini ya shilingi milioni 180 ndani ya saa 24 baada ya kubainika kupokea na kuchakata samaki wasioruhusiwa kwa kukiuka Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 sambamba na Sheria ya usimamizi wa Mazingira namba 20 ya mwaka 2004
Pia Waziri Mpina amechukizwa na kitendo cha viwanda hivyo kufadhili uvuvi haramu na kueleza kuwa ni bora kutokuwa na kiwanda hata kimoja cha samaki kuliko kuendelea kuwa na viwanda vinavyofadhili uvuvi haramu na kutishia kuvifunga viwanda vyote sambamba na kutaifisha samaki, magari na boti zinazobeba samaki wasioruhusiwa.
Waziri Mpina amesema hayo jana kwa nyakati tofauti wakati alipofanya ziara kutembelea viwanda vinavyochakata samaki jijini Mwanza ambapo pia alimuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Yohana Budeba kuwasimamisha kazi maofisa watatu wa Kitengo cha Udhibiti wa Usalama na Ubora wa Mazao ya Uvuvi Kituo cha Mwanza kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kulisababishia Taifa hasara kubwa.
Maofisa hao ambao Waziri Mpina ameagiza wasimamishwe kazi na kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu ni pamoja na Philemon Mugabo,Dorina Mlenge na John Bosco Rubajuna
Waziri Mpina ametaja viwanda vilivyokutwa vikichakata samaki wasioruhusiwa wakiwemo samaki wazazi na samaki wachanga na idadi ya kilo zilizokamatwa kwenye mabano kuwa ni pamoja na Nile Perch Fish (920), Victoria Fish (131), Nature Fish (150), Omega Fish (580), Tanzania Fish Processing (842) huku magari 41, boti 15, Nyavu haramu 294 wakiwa na samaki wachanga na wazazi ambapo sheria inakataza kuvuliwa samaki chini sentimita 50 na juu ya sentimita 85 .
Majina ya viwanda hivyo na faini zao walizotozwa Nile Perch sh milioni 25, Tanzania Fish Processing sh. milioni 50, Victoria Perch Milioni 30, Nature Fish milioni 25, Omega Fish Ltd milioni 50 ambapo amesisitiza kuwa adhabu hiyo ni ya kwanza na ya mwisho na kwamba ikithibika tena wenye viwanda waendelea kufadhili uvuvi haramu hatua za kuvifunga viwanda na kutaifisha mali ikiwemo mitumbwi, boti na magari yatakayokuwa yanabeba samaki hao itafuata.
Waziri Mpina amesema ukanda wa Ziwa Victoria ulikuwa na Viwanda 13 vya kuchakata samaki vilivyokuwa na uwezo wa kuchakata tani 1,065 kwa siku lakini kutokana na kushamiri kwa uvuvi usiongatia sheria kumesababisha viwanda 5 kufa kutokana na kukosekana malighafi na kwamba viwanda 8 vilivyobaki sasa vinachakata tani 171 tu kwa siku huku ajira zikiwa zimeporomoka kutoka ajira 4, 088 na kufikia 2,179 tu.
Mpina amesema tayari Rais Dk John Magufuli ameshatoa maagizo kwa wavuvi kuachana na uvuvi haramu sambamba na wenye viwanda kutofadhili uvuvi huo huku pia Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan naye akisisitiza jambo hilo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikikemea vikali huku Sheria za nchi nazo zikikataza jambo hilo lakini wenye viwanda kwa makusudi wameamua kudharau maagizo ya viongozi wakuu wa nchi jambo ambalo Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya uongozi wake Waziri Mpina haliwezi kukubalika kamwe.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dk. Yohana Budeba amesema kama watumishi wa wizara yake wangesimamia majukumu yao kikamilifu mambo hayo aliyobaini Waziri Mpina yasingejitokeza huku akikiri kupokea maagizo yake yote na atayasimamia kwa haraka kuona yanatekelezwa.
Afisa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC), Mhandisi Boniphace Guni amesema wenye viwanda hivyo wamekutwa na makosa ya kupatikana na samaki waliochini wa ukubwa, kukutwa na samaki wachanga kinyume cha Sheria ya Usimamizi Mazingira namba 20 ya mwaka 2004 pamoja na Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 ambapo wamekiuka kifungu namba 58(I)(a) hivyo wamestahili adhabu hiyo ya kulipa faini ya milioni 180 ndani ya saa 24
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina akimbeba samaki aina ya sangara aliyevuliwa kinyume na taratibu alipokuwa katika ukaguzi wa mazao ya uvuvi katika Kiwanda cha Nature Fisheries Limited Jijini Mwanza, kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Yohana Budeba na kulia ni Afisa Uvuvi Mkuu Bw. Boniface Shatila.
Samaki mzazi aina ya Sangara aliyevuliwa kinyume na taratibu(alikuwa na urefu wa sentimita 120), samaki ambaye akiachwa ziwani kwa muda wa miezi mitatu ana uwezo wa kuzaa samaki milioni tatu, na kuongeza idadi kubwa ya jamii
hiyo ya samaki katika ziwa Victoria.
Samaki chini ya sentimita 50 na mwenye zaidi ya sentimita 85 hawaruhusiwi kisheria kuvuliwa.