Watu wawili wameuawa wilayani Kalambo mkoani Rukwa katika matukio tofauti, likiwamo la mtoto kuuawa kwa kupigwa ngumi na mateke tumboni na baba yake.
Katika tukio la kwanza lililotokea Januari 1 saa 4 usiku, mtoto Benedicto Salumu (13), mkazi wa Kitongoji cha Saint Maria Kata ya Matai wilayani humo, inadaiwa alipigwa na baba yake hadi kufa baada ya ugomvi kuzuka kati ya mama na baba wa mtoto huyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Rafael Sinyangwe, kwa muda mrefu kumekuwapo ugomvi baina ya baba wa mtoto, Pius Salum (46) na mkewe, Hilda Mpangamila (37), akimtuhumu mkewe kuwa mtoto huyo si wa kwake.
Mwenyekiti huyo alisema Salum mara kadhaa amekuwa akiwalalamikia ndugu zake kuwa mkewe alibeba ujauzito wa mtoto huyo wakati akiwa amekwenda kutafuta maisha na aliporudi alihisi mkewe ni mjamzito.
Sinyangwe aliongeza kuwa tofauti hizo zilisababisha mvutano mkubwa wa mara kwa mara kati ya wanandoa hao.
Mwenyekiti Sinyangwe alidai siku ya tukio hilo mtuhumiwa akiwa ametoka kusherehekea Mwaka Mpya, aliingia chumbani na kukuta mtoto huyo akiwa amelala kisha kuanza kumpiga na ngumi na mateke sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwamo tumboni hadi kusababisha kifo chake.
Aliendelea kudai kuwa baada ya kumua, alimpiga pia mke wake akidai amemsababishia kulea mtoto asiyekuwa wake kwa muda mrefu, hali mbayo ilikuwa ikimuudhi na kumkosesha amani.
Katika tukio jingine lililotokea Januari 1 majira ya jioni, mkazi wa Kijiji cha Kafukoka kata ya Kisumba wilayani Kalambo mkoani Rukwa Kalasto Katanti (40) aliuawa na ndugu zake baada ya kipigo kikali wakidai kuchukizwa na madeni aliyonayo.
Kabla ya kuuawa kwa kipigo Katanti alikuwa anadaiwa shilingi 64,000, deni ambalo lilikuwa ni la muda mrefu kiasi ambacho alionekana ameshindwa kulilipa.
Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Frank Sichalwe, alisema ndugu zake wawili ambao ni Florens Zunda (38) na Dafusi Zunda (35) ndipo walipoamua kumpiga hadi kumuua wakidai wamechoshwa na tabia yake ya kukopa fedha wakati anajua hana uwezo wa kulipa, kitendo kinachodhalilisha ukoo wao.
Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, George Kyando, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na Kuongeza kuwa watuhumiwa wanashikiliwa na polisi na watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazo wakabili.