SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 10 Januari 2018

T media news

Serikali Kuzipokonya Leseni Benki Ambazo Hazitajiunga Na Mfumo Wa Kielektroniki Wa Kukusanya Mapato Ifikapo Januari 31, 2018

Na. WFM

Benki zote nchini Tanzania na Kampuni za Mawasiliano zinatakiwa kuwa zimejiunga na mfumo wa wa Kielektroniki wa kukusanya mapato kupitia kituo cha Data kilichopo Kijitonyama Jijini Dar es Salaam ifikapo Januari 31, 2018 kinyume na hapo Serikali itanyang’anya Leseni za uendeshaji wa shughuli zao hapa nchini.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) alipokutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Benki Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa mwaka 2017 zilitungwa Kanuni za Sheria za utawala wa Kodi ambao ulizitaka Benki na Kampuni za Simu kuwa zimejiunga na Mfumo wa kielektroniki wa kukusanya kodi kati ya Juni, 2017 hadi Desemba 31, 2017 na mpaka sasa ni Benki 27 tu ambazo zimetekeleza hatua hiyo ya Kisheria.

‘Nimekutana na Benki takribani 20 ili kuwasikiliza ni kwanini hawajatekeleza matakwa ya sheria na katika mjadala huo nimebaini sababu kadhaa zilizosababisha baadhi ya Benki kuchelewa kuchukua maamuzi, miongoni mwa sababu hizo ni hofu kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ambayo inaweza kuona miamala na hivyo kuweza kusababisha wizi wa kimtandao” alieleza Dkt. Mpango.

Sababu nyingine ni pamoja na Matakwa hayo kuja ghafla hivyo kuhitaji fedha za dharula na Benki kubwa kama City Bank kuwa na mtandao mkubwa Kimataifa wa nchi takribani 100 hivyo kuwalazimu kuwasiliana na Makao Makuu ya Benki hiyo kabla ya kufanya Maamuzi.

Hata hivyo kwa kuwa tayari wamevunja sheria iliyowataka kutekeleza agizo la Serikali kufikia Desemba 31, 2017, Waziri Mpango amemuagiza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Charles Kichere kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo faini katika kipindi walichoshindwa kutekeleza sheria.

Dkt. Mpango amezipongeza Benki zilizotekeleza Sheria ndani ya muda uliowekwa kuwa ni pamoja na Exim Bank, Benki ya NMB, Benki ya Posta, Amana Benki, CRDB, China Comnercial Bank, Stanbic na Akiba Commecial Bank na nyingine.

Benki ambazo zipo katika hatua nzuri ni pamoja na I&M, DCB, DTB, Mkombozi Bank, Maendeleo Bank wakati Benki ambazo hazijapiga hatua kuwa ni pamoja na Bank of Africa, Yetu Microfinance Bank, Barclays na Mwanga  Rural community Bank.

Kwa upande wa Mikopo Chechefu katika Benki, Waziri Mpango ameeleza kuwa  hali haikuwa nzuri kwa mwaka 2017 kwa kuwa Mikopo Chechefu ilifikia asilimia 12 ya mikopo yote ya Sekta ya Benki ambapo kwa sasa Wadau wa Benki wameona kuna hatua nzuri katika eneo hilo hivyo kufanya Sekta hiyo kuimarika.

Ameeleza kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iko imara na Sekta ya Benki kwa sasa ina ukwasi wa kutosha na si kweli kama mikopo chechefu inaiangusha sekta hiyo.

Amezitaka Benki  nchini kuwa na mfumo mzuri unaofuata taratibu za mikopo ili kutatua tatizo hilo kwa kukopesha watu wenye vigezo na pia Mahakama imetakiwa kuheshimu dhamana za awali zilizowekwa na wakopaji kwa kuwa kuna wanaokubaliwa dhamana zao na baadaye Mahakama inasema dhamana hizo hazipo halali jambo linaloongeza uwepo wa mikopo hiyo chechefu.

Mwisho.