Watu saba akiwamo ofisa wa ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Ziwa, Rwige Ogunya wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza kujibu mashtaka ya uhujumu uchumi baada ya kukutwa na mapipa 200 yenye ujazo wa lita 50,000 za kemikali bashirifu inayodhaniwa kuwa ni ethyl alcohol.
Pamoja na Ogunya, wengine waliosomewa shtaka namba 1/2018 la Uhujumu Uchumi ni Mwita Ikohi, Cholla Maginga, Jamal Kulusanga na Eunice Mazinge ambao kwa pamoja walidaiwa kukutwa wakisafirisha mapipa hayo kinyume cha sheria.
Mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Gwaye Sumaye mwendesha mashtaka wa Serikali, Seth Mkemwa alisema kosa hilo ni kinyume cha kifungu cha 15 (ib) cha sheria namba tano ya mwaka 2015 ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016, na mabadiliko madogo ya mwaka 2017.
Akisaidiana na mwenzake, Gastus Namgoba, Mkemwa alimwambia Hakimu Sumaye aliyesikiliza shauri hilo kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Wilbert Chuma kuwa tukio hilo lilitendeka Desemba 13, 2017 katika eneo la kivuko cha Kigongo wilayani Misungwi mkoani Mwanza.
Katika shtaka namba 2/2018 la uhujumu uchumi, washtakiwa Emmanuel Munis (38) na Samwel Petro (28) wanakabiliwa na kesi ya kujihusisha na biashara haramu ya kemikali bashirifu kinyume cha kifungu cha 15 (ib) cha Sheria Namba Tano ya mwaka 2015 ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016, na mabadiliko madogo ya mwaka 2017.
“Mnamo Desemba 20, mwaka 2017 katika eneo la Kiseke ‘A’ wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, washtakiwa kwa pamoja walitenda kosa la kukutwa na lita 414 za kemikali bashirifu inayodhaniwa kuwa ni ethyl alcohol,” alidai Mkemwa
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashauri hayo na walipelekwa mahabusu ya Gereza Kuu la Mkoa wa Mwanza, Butimba hadi Januari 22, kesi zao zitakapotajwa tena mahakamani hapo.