SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 4 Desemba 2017

T media news

Mtoto Aliyedhaniwa ni wa Kike kwa Miaka 7 Abainika Kuwa wa Kiume

Mtoto wa miaka saba aliyelelewa kama mtoto wa kike kutokana na maumbile yake kutoeleweka vema, baada ya vipimo vyote katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ameonekana kuwa ni mwanamume, hivyo amefanyiwa upasuaji wa kwanza wa kushusha kokwa (mbegu za kiume) kwenda kwenye korodani ili kumrejesha katika hali ya kawaida.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto MNH,  Zaitun Bokhary alisema hayo alipofanya mahojiano maalumu na gazeti la HabariLeo kuhusu kambi ya wiki moja iliyowekwa kwa ajili ya kufanya upasuaji ambao ni mgumu, wakishirikiana na wataalamu watano kutoka Chuo Kikuu cha Oxford nchini Marekani.

Dk Bokhary alisema upasuaji huo ni hatua ya kwanza katika kumrejesha mtoto huyo katika hali ya kawaida, hatua nyingine za upasuaji zitafuata, kwani atafanyiwa upasuaji kwa hatua tatu.

Alisema kwa kuwa mtoto huyo vipimo vimeshaonesha kuwa ni wa kiume, wametoa ushauri kwa wazazi wake hususan baba yake kuwa karibu na mtoto huyo ili kumfanya asijisikie vibaya, kwani awali alikuwa akijisaidia haja ndogo kama mtoto wa kike, pia alikuwa amepewa jina la kike ikiwa ni pamoja na kuvaa nguo za kike.

“Tumemshauri baba yake kutembea mara kwa mara na mtoto wake, pia kwenda naye katika michezo ya kiume, ikiwa ni pamoja na kuanza kumvalisha mavazi ya kiume. “Mtoto huyu alipoanza kuvaa nguo za kiume kwa mara ya kwanza alikuwa akijisikia aibu kwa kuwa alishazoezwa mambo ya kike, lakini tunaendelea kutoa ushauri kwa wazazi ili wawe karibu na mtoto wao asijisikie tofauti yoyote,” alisema daktari huyo.

Aliongeza kuwa kwa kuwa tayari mtoto huyo alikuwa akisoma katika shule ya msingi mojawapo jijini Dar es Salaam, hospitali hiyo inafanya utaratibu kupitia kwa daktari wake ili kuandika barua kwa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita), atambuliwe kama mwanamume, ikiwa ni pamoja na kuhamishwa shule aliyokuwa akisoma.

Alisema kuwa na sasa mtoto huyo, amehamishwa nyumbani kwao anakaa na ndugu zake eneo lingine ili aanze kuzoea mazingira mapya ya maumbile yake. Pia Dk Zaitun alielezea upasuaji mwingine mgumu uliofanyika ni wa mtoto wa siku mbili ambaye alikuwa na tatizo katika mfumo wa nyongo, njia ilikuwa imefungwa ilibidi apasuliwe kufungua njia ili mfumo wa nyongo uendelee kama kawaida.

“Kwenye mfuko wa nyongo kulikuwa kumetengeneza uvimbe nyongo isipite vizuri, hivi sasa baada ya upasuaji anaendelea vizuri,” alisema. Daktari bingwa huyo wa upasuaji wa watoto, alieleza upasuaji mwingine walioufanya ni kwa mtoto aliyekuwa na saratani ya figo zote mbili, moja ilitolewa na nyingine ilikuwa haijalika ikaondolewa sehemu ya tatizo bila kuathiri mfumo wa misuli.

Alisema upasuaji wote huo umekwenda vizuri, hali za watoto hao zinaendelea vema. Alisema kambi ya upasuaji huo ilikuwa Novemba 27 hadi Desemba Mosi, mwaka huu iliongozwa na Daktari Bingwa Mshauri Mwelekezi wa Upasuaji wa Watoto, Profesa Kokila Lakhoo kutoka Chuo Kikuu hicho cha Oxford. Alisema Dk Lakhoo amekuwa akija hospitalini hapo kila mwaka, kusaidia ule upasuaji ambao ni mgumu, na huu ni mwaka wake wa tano kufika nchini.

Chanzo: HabariLeo