Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Gilliard Ngewe ameeleza kuwa madereva na makondakta watakaoruhusu mijadala hiyo pamoja na wafanyabiashara watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria kwani vitendo hivyo huwabugudhi abiria.
“Kuruhusu watu waanze siasa, mahubiri, mambo ya kwao, wanapiga kelele…. hapa ni dereva au kondakta wa lile basi ndio tutamchukulia hatua,” alisema Mkurugenzi Ngewe.
Aliongeza kuwa madereva na kondakta wwe waangalifu na aina ya miziki pamoja na video zinazoonyeshwa ndani ya basi na wahakikishe kuwa ni ile inayoruhusiwa na mamlaka husika kuonyeshwa hapa nchini.
“Muziki basi ufuate yale maadili, kuna vyombo ambavyo vinaangalia miziki na video za aina gani zinaruhusiwa nchini basi hakikisha ni ile ambayo imepitishwa na vile vyombo,” alisema.
Aidha Mkurugenzi Ngewe alieleza kuwa ili basi liruhusiwe kutoa huduma ya usafiri kwa abiria hapa nchini lazima mmiliki ahakikishe basi lake halina ubovu na linafanyiwa matengenezo yanayohitajika kila mara, basi linatakiwa kubeba idadi ya abiria ambao wameandikwa kwenye kasi ya gari na leseni yake na Dereva wa basi hatakiwi kuendesha masaa zaidi ya nane mfululizo, hivyo kwa mabasi yanayokwenda safari ndefu mf. kilomita 1200 inabidi yawe na madereva wawili.