Mbunge wa upinzani nchini Zimbabwe Eddie Cross ameambia BBC kwamba anaamini mke wa Rais Mugabe, Grace, ametorokea Namibia.
Mwanasiasa huyo wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) amesema anafahamu kwamba Grace aliruhusiwa kuondoka nchini humo usiku wa kuamkia leo na jeshi.
Ameongeza kwamba alikuwa hana kwingi kwa kwenda kutafuta hifadhi baada yake kudaiwa kumdhalilisha mwanamitindo Afrika Kusini jambo lililomaanisha kwamba hawezi kuwa salama huko.
Hata hivyo, taarifa hizi hazijathibitishwa na jeshi.
Nick Mangwana, mwakilishi wa chama tawala cha Zanu-PF nchini Uingereza ameambia BBC kwamba mwenyewe pia amepokea taarifa kwamba Grace hayupo tena nchini Zimbabwe.
Lakini Bw Mangwana amesema katika siasa za Zanu-PF, Bi Mugabe ni mtu wa chini sana na hana usemi wowote.
Amesema ana mamlaka tu kwa sababu ya kuwa ni mke wa Rais Mugabe.
„Alichukua wadhifa wa juu kuliko ule anaostahiki kuwa nao,” amesema.