SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 15 Novemba 2017

T media news

Sina Uwezo wa Kulipa Milioni 250 Kilichobaki ni Kujiandaa Kisaikolojia Kufungwa Jela- Babu Tale

Wakati siku 14 zilizotolewa na kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart & Co Ltd, kwa wakurugenzi wa kampuni ya Tip Top Connection Limited kutekeleza amri ya Mahakama zikikaribia kuisha, Hamis Taletale (Babu Tale), amejitetea huku akidai kuwa anajiandaa kisaikolojia kwa kifungo.

Babu Tale ambaye pia ni meneja wa msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Diamond Platnum, pamoja na nduguye Iddy Taletale ni wakurugenzi na pia wanahisa wa kampuni hiyo.

Februari 18, 2016, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliiamuru kampuni hiyo kumlipa fidia ya Sh250 milioni Mhadhiri wa Dini ya Kiislam Sheikh Hashim Mbonde, kwa kutumia kibiashara mahubiri yake bila ridhaa wala makubaliano.

Babu Tale amekiri kupokea taarifa hiyo ya Yono, lakini akasema kuwa yeye hajui chochote kuhusu madai hayo, kwani hakuwahi kujihusisha  na kampuni hiyo na kwamba hana cha kufanya bali anawasubiri kuona Yono hizo siku walizopewa ili waone hatua zitakazofuata.

“Lakini mimi nasema sijamdhulumu huyo mzee wala sijawahi kufanya naye biashara. Kwa kuwa hiyo ni amri ya Mahakama sawa sina cha kufanya, kama watasema tulipe nitaeleza uwezo wangu maana mimi sina uwezo huo wa kulipa hizo Sh250 milioni,” amesema na kuongeza:

“Kwa hiyo cha kufanya ni kujiandaa tu kisaikolojai hata kama ni kufungwa, kwani hata kina Mandela (Nelson) walifungwa jela hivyo hivyo.”

Amesema kuwa kampuni hiyo ilifunguliwa na ilikuwa ikimilikiwa na kaka yao Abdul Taletale (marehemu kwa sasa) kwa asilimia miamoja na kwamba baada ya kufariki kampuni hiyo haikuendelea na mali zake zote zilipotea kwani zilidhulumiwa.

Amesema kuwa japo anatajwa kama mhusika lakini hakuwahi kuwa mkurugenzi, mwanahisa wala kujihusisha kwa namna yoyote na kampuni hiyo na kwamba  hakuona taabu kwani hakujua kama kuna siku yatatokea matatizo kama haya.

Ameongeza kuwa alifahamu kuwepo kwa kesi hiyo baada ya kaka yao kufariki, ambapo wakili wa mdai alimpigia simu akimtaka afike mahakamani, lakini yeye alipuuza kwa kuwa alijua si mhusika.

Kwa mujibu wa hukumu ya kesi ya msingi ya madai namba 185 ya mwaka 2013, Juni 6, 2013 Sheik Mbonde aliingia makubaliano na kampuni hiyo, kutumia kazi zake za mawaidha, kwa kuzalisha, kurekodi na kuzisambaza na kugawana faida ya mauzo.

Hata hivyo, baada ya kukamilisha kurekodi masomo saba, kampuni hiyo ilimkatia mawasiliano hadi alipobahatika kukutana na ofisa mmoja wa kampuni hiyo,  Adam Waziri ambaye alimweleza kuwa wamesitisha mpango huo.

Lakini Agosti 9, 2013, wakati mdai akiendesha mhadhara Bahi Dodoma, alibaini kuwa DVD za masomo yake zilikuwa zikiuzwa sokoni Dodoma na katika  mikoa mbalimbali, bila ridhaa yake wala makubalino ndipo akafungua kesi hiyo.
Chanzo:Mwananchi