Wanafunzi watano wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kihinga wilayani Ngara mkoani Kagera wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa baada ya kulipukiwa na kitu kinachoaminika kuwa bomu.
Mlipuko huo umetokea leo Jumatano Novemba 8,2017 asubuhi wanafunzi hao walipokuwa wakiingia darasani.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Misheni Rulenge, Goreti Francis amethibitisha kupokewa miili mitatu na majeruhi 20.
Kati ya majeruhi hao, amesema wawili walifariki wakati wakipatiwa matibabu.
“Majeruhi wana majeraha sehemu mbalimbali za mwili, tunafanya kila jitihada kuokoa maisha yao,” amesema Dk Francis.
Akizungumza kwa simu akiwa eneo la tukio, zaidi ya kilomita 50 kutoka Ngara mjini, diwani wa Kibogora, Adronis Bulindoli amesema wanafunzi waliofariki wana umri kati ya miaka minane na tisa.
Amesema askari polisi kutoka Kituo Kidogo cha Kata ya Bugarama kwa kushirikiana na maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wa kikosi cha kulinda mpaka kilichopo Bugarama wanaendelea na uchunguzi eneo la tukio.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Ollomi na viongozi wengine wa wilaya kuzungumzia tukio hilo zimeshindikana kwa kuwa wapo kwenye msafara wa Rais John Magufuli aliye ziarani mkoani Kagera.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Erick Nkilamachumu amesema kuna hisia kuwa mmoja kati ya wanafunzi hao alibeba mlipuko unaodaiwa kuwa ni bomu baada ya kuliokota.
Kata ya Bugarama ambako Shule ya Msingi Kihinga ipo ni miongoni mwa maeneo yanayopakana na nchi jirani ya Burundi ambayo imekuwa na mapambano kuhusu madaraka.