Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amependekeza serikali ya muda iundwe nchi humo na kutawala kwa muda wa miezi sita kama sehemu ya kutatua mzozo wa kisiasa nchini humo.
Bw Odinga, ambaye alisusia uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi uliopita, amesema katika kipindi hicho kunafaa kufanyika marekebisho ya katiba kuchunguza upya mamlaka ya rais.
Kiongozi huyo ambaye ameanza ziara nchini Marekani alisema yuko tayari kufanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu marekebisho ya kikatiba ambayo anasema yanahitajika kupunguza hatari ya kuzuka kwa fujo kutoka kwa makundi ya jamii za wachache ambao wanajiona kwamba wametengwa.
Bw Kenyatta alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo wa marudio uliofanyika tarehe 26 Oktoba akiwa na kura 7.5 milioni ambazo ni sawa na asilimia 98 ya kura zilizopigwa.
Waliojitokeza kushiriki uchaguzi huo ni asilimia 39 ya waliojiandikisha kuwa wapiga kura nchini humo.
Uchaguzi huo ulitokana na hatua ya Mahakama ya Juu, kufuatia kesi iliyowasilishwa na Bw Odinga, kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa tarehe 8 Agosti ambapo Bw Kenyatta alikuwa ametangazwa mshindi akiwa na asilimia 54 ya kura.
Mahakama ya Juu ilisema uchaguzi huo wa mwanzo ulikumbwa na kasoro nyingi.
Bw Odinga alisusia uchaguzi wa marudio akisisitiza lazima mageuzi yafanywe katika Tume ya Uchaguzi (IEBC).
Alisema hakuna na imani kwamba uchaguzi huo wa marudio ungekuwa huru na wa haki.
Wafuasi wa Bw Odinga wamekuwa wakiandamana mara kwa mara tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa kwanza.
Watu zaidi ya 50 wameuawa katika makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa upinzani.
"Mfumo halisi wa utawala wa urais unaendeleza ukabila kwa sababu kila kabila linahisi kwamba haliko salama ikiwa mtu kutoka kabila hilo si kiongozi," aliambia Reuters kwenye mahojiano.
Katiba mpya iliyoanza kutekelezwa mwaka 2010 iligatua baadhi ya mamlaka ya serikali kuu kwa kuunda serikali za majimbo 47 zinazoongozwa na magavana.
Serikali hizo huwa na uwezo wa kujiendeshea shughuli nyingi lakini bw Odinga anasema mamlaka mengi bado yamebaki kwenye serikali kuu na hilo linafaa kubadilika.
"Tulipata katiba mpya mwaka 2010; Tunafikiri kwamba wakati umefika tuiangalie upya," amesema.
Alieleza kuwa marekebisho ya Katiba hiyo yanafaa kuimarisha taasisi huru za serikali mfano tume ya uchaguzi na kupunguza mamlaka ya rais.
"Tunafikiri kwamba pengine miezi sita itatosha kufanikisha marekebisho haya ambayo tunayahitaji katika taifa hili," alisema.
Bw Kenyatta, baada ya kutangazwa mshindi, alisema hatafanya mazungumzo na upinzani hadi umalize njia zote za kisheria za kupinga matokeo ya uchaguzi.