Sarah Joseph
Huyu anatokea katika familia ya Kikatoki ya Uingereza ambayo mizizi yake inatokana na uvamizi wa Norman (Norman Conquest). Mama yake alianzishaa uwakala wa kwanza wa mitindo Uingereza na Joseph anadai kuzunguukwa na watu wazuri zaidi hapo katika ofisi za mitindo mtaani kwao.
Mtoto huyu Mkatoliki babake akiwa mhasibu na mamake aliyekuwa mwanamitindo anakumbuka alivyokuwa na umri wa miaka 14 akimkimbilia Naomi Campbell akiwa na kadi ya biashara ya mama yake. Na katika kipindi kifupi baadae, kaka yake akawa Muislamu. Akijilazimisha kupingana na chuki zake kwa Waislamu, Sarah akaanza kusoma dini. “Taratibu, Uislamu uliendelea kunijibu maswali yangu ambayo yalinitatiza mpaka pale nilipoutaka Uislamu wenyewe,” anasema. Na alivyotimu miaka 17, Sarah alibadili dini kuwa muislam, akiukana Ukatoliki aliolelewa nao. Akaamua kuwa mvaaji hijab, vazilililompa ukombozi na taadhima. “Nataka nihukumiwe kwa kile ninachosema, na sio kwa vile ninavyoonekana,” alishawahi kusema hivi.
Katika mahojiano na Gabrielle Procter, Sarah Joseph alisema:
“…Kuwa Muislamu kunakupa haiba nzuri lakini kubwa zaidi sasa ni binaadamu kikwelikweli. Nimeishi miaka 16 nikiwa sio muislam, sasa hivi mimi kama mwanadamu, mwanamke, mama, mhariri, na mwenyeji wa London- vyote hivi vinanisaidia. Lakini jukumu langu kama mama linanyooshwa na kuwa Muislamu; kazi yangu kama mhariri, na ufahamu wangu kama mmoja wa wanajamii vyote vinanyooshwa na falsafa yangu hii mpya… mimi ni mtu wa imani na naamini mtu wa imani yapasa awe na matumaini. Nawaona vijana wengi wanaojumuika katika jamii mbali mbali za kiengereza wakiwa waerevu, fasaha, wenye msukumo wa kuleta tija katika jamii yao na wakiwa sehemu ya jamii ya kiislamu. Nadhani Waislamu wana uwezo wa kuchangia pakubwa katika jamii. Na kama watu ikatokea wauone uislam ni sehemu ya utatuzi badala ya kuuona ni sehemu ya tatizo, wataishi kwa raha mustarehe.”
Sarah amepata shahada yake ya kwanza katika masomo ya dini kutoka Chuo Cha King cha London. Alifanya utafiti kuhusu Waingereza Wanaosilimu akisomea shahada yake ya pili. Pamoja na hilo, amekuwa mshindi wa 1999-2000 wa shani ya kusomeshwa bure kutoka katika mfuko wa King Faisal Foundation/ Prince of Wales Chevening. Ni mhariri wa jarida la Emel (jarida la kiislamu linalosomwa zaidi Uingereza- jina lake linasomeka M na L likisimama badala ya Muslim Life (Maisha ya Muislam), likimaanisha ‘tumaini’ kwa lugha ya Kiarabu). Pia ni mtangazaji wa British Muslims, na ni mwandishi. Sasa, akisomea shahada nyengine amekuwa akifanya kazi kwa muda kama mwalimu wa chuo ambaye amekuwa akifanya mihadhara mingi na sehemu nyingi inayohusiana na masuala ya dini na wanawake. Mwaka 2004, alitunukiwa OBE (Tuzo ya Uingereza inayosimama badala ya Order of the British Empire), kwa mchango wake katika midahalo ya dini. Sarah kashajumuika katika vipindi vingi vya televisheni za Uingereza vikiwemo –Panorama naJohnathan Dimbleby. Pamoja na kufanya kazi kama mtafiti mzoefu katika kitengo cha kujifunza cha BBC 2001 Islam Series.
Pia amekuwa mhariri mkuu wa kwanza mwanamke wa gazeti kubwa la Waislamu: Trends. Sara Joseph ni mhariri muanzilishi wa baraza la Waislamu la Uingereza The Common Good Consultant on Islamic Affairs– likishughulika na utafiti na mafunzo kwa wale wanaoihitaji kuajiriwa, kusoma, kuwa na afya bora, polisi n.k. katika misingi ya Kiislamu.
Ameolewa na Mahmud ar-Rashid, mwanaharakati wa haki za binadam. Miongoni mwa vyama vya vijana na jamii ambavyo ar-Rashid anaongoza ni: the Muslim Council of Britain (MCB), baraza kuu la kutetea Waislamu Uingereza na ni pia mwenyekiti Islamic Society of Britain. Wana watoto watatu tayari: Hasan, Sumayyah na Amirah.
Akiongelea kuhusu makundi ya watu wanaoingia katika Uislamu kila kukicha, hususan kwa kutumia makadirio ya watu 10,000 mpaka 50,000 wanaoingia katika Uislamu kila mwaka Uingereza, Sarah anadhani kufikia mwaka 2020, Uislamu itakuwa ndio dini inayofatwa zaidi Uingereza, “Sisi ni wa pili kwa kuwa na idadi ya wafuasi wengi Uingereza ila ifikapo 2020 tutakuwa tunaongoza rasmi kwa kuwa na waumini wengi wahudhuriaji ibada zao kama ukitumia uhudhuriaji wa kanisa na msikiti kama kigezo,” Alisema hayo kuiambia GDN.