SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 12 Septemba 2017

T media news

Ukaribu wa Mwigulu Yanga na Singida United utaathiri matokeo uwanjani? Mkurugenzi amejibu

Ukitaja sifa tano za Waziri Mwigulu Nchemba huwezi kuiacha ya unazi wake kwa klabu ya Yanga, kitu kizuri ni kwamba hata yeye mwenye huwa hajifiji inapofikia suala la uyanga wake kwenye ushabiki wa soka.

Sasa Waziri Nchemba kwa sasa ni miongoni mwa wadau wakubwa wa Singida United mwenye anasema mbali ya kuwa sehemu ya wamiliki wa Singida United  lakini timu hiyo ni ya nyumbani kwao Singida hivyo hakuna namna ni lazima awe karibu nayo.

Sasa watu wanajiuliza uyanga wa Mh. Nchemba na ukaribu wake na Singida United hauwezi kuathiri matokeo uwanjani hususan pale Yanga inapokuwa inahitaji pointi muhimu za kuamua ubingwa halafu inakutana na Singida United vivyo hivyo endapo Singida itahitaji pointi halafu mechi inayofuata ni dhidi ya Yanga?

“Singida United inaendeshwa kwa mfumo wa kampuni kwa hiyo tunafanya kazi bila kuingiliwa na mtu ndio maana tupo straight, tumemweleza Mh. Nchemba kwamba yeye kuwa karibu na Yanga pamoja na Singida United kusiathiri timu yetu uwanjani hasa linapokuja suala la matokeo,” Festo Sanga-Mkurugenzi Singida United.

“Sisi target yetu ya kwanza ni kuchukua ubingwa, kuna vilabu ambavyo vinamiliki mpira wa Tanzania  lakini sisi tunataka kuonesha watanzania na ulimwengu tunaweza kuwa klabu kutoka nje ya Dar kufanya jambo fulani nje ya Simba na Yanga.”

Kocha wa sasa wa Singida United Hans van der Pluijm alikuwa kocha wa Yanga kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na George Lwandamina, inakumbukwa namna Mwigulu alivyopambana kuhakikisha Pluijm anarejea Yanga baada ya awali kujiuzulu kufuatia tetesi za ujio wa Lwandamina ndani ya klabu hiyo.