Afisa Habari wa klabu ya Simba amethibitisha kwamba Haruna Niyonzima ni mchezaji halali wa klabu hiyo mara baada ya kumaliza mkataba na klabu yake ya zamani Yaga ambayo aliichezea hadi msimu uliopita.
Kulikuwa na tetesi nyingi kuanzia kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na hata kwa wadau mbalimbali kuhusu Niyonzima kusainiwa na Simba lakini klabu hiyo haikuthibitisha mapema hilo.
“Haruna Niyonzima ni mchezaji halali wa Simba tumeshamalizana nae, ameshamaliza mkataba na club aliyokuwa anaitumikia atakuja Simba. Anaweza akaenda South Africa kuungana na kikosi au anaweza kuja moja kwa moja Dar katika safari moja na Rayon Sport na atacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Rayon Sports siku ya Simba Day,” – Haji S. Manara Afisa Habari Simba SC.
“Ana mambo binafsi ambayo anayashughulikia na anayamaliza pale Kigali, atakuja wala hakuna shaka na hatuzungumzi kwa kificho. Pamoja na kuwa na mambo yake uko kwao lakini anafanya mazoezi na timu ya APR, sidhani kama tutaulizwa tena kuhusu Haruna.”
Yanga tayari walishatoa taarifa mapema kwamba hawakufikia makubaliano na Niyonzima baada ya star huyo wa Rwanda kutaka dau kubwa ili aongeze mkataba mpya wa kubaki Yanga.
Kwa sasa Niyonzima yupo Rwanda mapumzikoni tangu kumalizika kwa ligi kuu Tanzania bara na kwa mujibu wa Manara, Niyonzuma ataungana na wachezaji muda wowote wiki hii.