SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 1 Agosti 2017

T media news

KUTOKA IKULU DAR


DAR ES SALAAM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 01 Agosti, 2017 amepokea hati za utambulisho wa Mabalozi watano walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho ni;
Mhe. Nguyen Kim Doahn – Balozi waVietnam hapa nchini.Mhe. Prof. Ratlan Pardede – Balozi waIndonesia hapa nchini.Mwadhama Askofu Mkuu Marek Solcynski–Balozi wa Vatican hapa nchini.Mhe. Dkt. Detlef Wachter – Balozi waUjerumani hapa nchini.Mhe. Richard Tumisiime Kabonero – Balozi wa Uganda hapa nchini.Akizungumza na Mabalozi hao Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na nchi hizo ambazo ni marafiki wa muda mrefu na washirika wa maendeleo wa Tanzania.
Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kutilia mkazo diplomasia ya uchumi kwa kuongeza juhudi za kuhamasisha wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo wa nchi hizo kushirikiana na Tanzania katika biashara na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda, kilimo na huduma za kijamii.
Kwa upande wao Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwapokea na wameahidi kuhakikisha uhusiano wa nchi zao na Tanzania unaendelezwa na kuimarishwa zaidi.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Benedict Martin Mashiba kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi.
Mhe. Benedict Martin Mashiba anachukua nafasi ya Mhe. Victoria Richard Mwakasege ambaye amestaafu.

Taarifa imetolewa leo na Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
01 Agosti, 2017