.MKONGWE wa muziki wa kizazi kipya, Dully Sykes ‘Mr Misifa’ amejinasibu kuwa anafanya sanaa hiyo kwa vile iko ndani ya damu yake na si kuganga njaa kama wengine wanavyofanya. Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, baba huyo wa watoto wanne, alisema familia yake yote imekuwa ikifanya muziki, kuanzia babu yake hadi baba yake.
“Mimi tangu babu yangu Mzee Wahed Abdul Sykes alikuwa mwanamuziki na Mwenyekiti wa chama cha muziki wa dansi Tanzania baba yangu pia alikuwa mwanamuziki, kwa hiyo Watanzania wengi wanafahamu kuwa mimi siyo mganga njaa, ni mwanamuziki mahiri mwenye uwezo wa kuimba na kupangilia mashairi. Alisema anachofahamu ni kwamba muziki umempa heshima, lakini siyo jina kwa
sababu familia yao imepata jina kubwa kupitia muziki tangu zamani.
“Siwezi kusema muziki ndiyo umenipa jina, hapa jina hili lilikuwepo tangu enzi hizo za babu yangu akitamba, lakini nasema muziki ndiyo umenifikisha hapa nilipo, hivi sasa nina studio yangu pale Tabata Kimanga nimeipa jina la 4.12,” alisema.
Aliongeza kuwa pamoja na kutoa vibao vingi katika muziki wake, lakini Wimbo wa Julieta ndiyo anaoukubali zaidi na akikisikia kibao hicho kinagongwa katika redio au chombo chochote kile lazima asimame akisikilize.