Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Sikika, Irenei Kiria, amesema hali ya kushuka kwa bei za dawa katika mahospitali pamoja na upatikanaji wa dawa nchini inaanza kuimarika ikilinganishwa na miaka iliyopita jambo ambalo ni faraja kwa wananchi.
Katika mahojiano na Wahariri wa vyombo vya habari amesema kuwa upatikanaji wa dawa katika Hospitali na vituo vya afya nchini umeongezeka kutoka asilimia 51 mwaka jana hadi kufikia asilimia 81 mwaka huu na bei ya dawa pia imeshuka kati ya asilimia 15 hadi 80, kwa mujibu wa taarifa ya bei ya dawa iliyotolewa na MSD hivi karibuni.
Alisema hali hiyo inatokana na vituo vya kutoa huduma za afya kuruhusiwa kununua dawa kutoka kwa wauzaji binafsi pindi zinapokosekana katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
“Kwa miaka kadhaa tumekuwa tukiishauri Serikali iondoe ukiritimba wa MSD kuwa sehemu pekee ya Hospitali na vituo vya afya kununulia dawa kwakuwa ndio chanzo cha kuadimika kwa dawa, kwani zikikosekana huko basi na sehemu za kutolea huduma zinakosa dawa. Sasa hivi vituo vimeruhusiwa kununua kutoka kwa wauzaji binafsi na hali ya upatikanaji wa dawa imekuwa nzuri,” alisema Irenei.
Alitoa mfano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, licha ya kununua dawa kutoka MSD, pia huagiza wenyewe nje ya nchi na kwa wauzaji wa ndani.
Aliongeza kuwa pamoja na maboresho yaliyofanyika, kitendo cha MSD kuwa mnunuzi na msambazaji pekee wa dawa bado ni changamoto, kwakuwa nchi ni kubwa kijiografia na vituo vya kutoa huduma za afya ni vingi.