Wajumbe wa kamati ya kuratibu rasilimali ya madini kwa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu wamepongeza Rais Dk John Magufuli kwa jitihada anazofanya za kudhibiti uvunaji haramu wa rasilimali hiyo na wamewaomba viongozi wa nchi zingine kuiga mfano huo.
Wakizungumza baada ya kumaliza kikao chao kilichokuwa kinafanyika mjini Arusha, wajumbe hao kutoka nchi 12 za Ukanda wa Maziwa Makuu walishauri jitihada zilizoonyeshwa na Rais John Magufuli zifanyike katika nchi zote za ukanda huo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha sheria zote za uchimbaji, uuzaji wa madini zinazingatiwa na nchi husika zinanufaika.
Mratibu wa kikao hicho kutoka sekretarieti ya nchi za ukanda huo, Balozi Zachary Muhuri Muita, alishauri uchimbaji wa madini ufanyike kwa njia halali na wachimbaji walipe kodi.