SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 2 Agosti 2017

T media news

Huduma za Kuhamisha Fedha Kwa Simu zaipaisha Tanzania kimataifa

HUDUMA ya M Pesa inayotolewa na kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom imetajwa kuwa chachu ya hatua kubwa iliyopigwa na Tanzania katika kuhakikisha watu wake wengi wanafikiwa na huduma za kifedha, imefahamika.

Kwa mujibu ripoti mpya ya Benki ya Dunia (WB) iliyopewa kichwa cha habari “Tanzania Economic Update: Money Within Reach, Extending Financial Inclusion” wakati M Pesa ikianza mwaka 2008, asilimia 16 tu ya Watanzania ndiyo ilikuwa na uhakika wa kupata huduma za kifedha lakini sasa asilimia 86 wanapata huduma hiyo.

“ Kulinganisha na nchi nyingine katika bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania imewaacha wenzake kwa mbali sana. Kutoka asilimia 16 hadi 86 katika kipindi cha chini ya muongo mmoja, hiyo ni hatua kubwa sana,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndullu, Vodacom kupitia M Pesa inashikilia asilimia 54 ya soko la huduma za kibenki kwa kupitia mawasiliano ya simu na kampuni nyingine ndiyo zinagawana asilimia iliyobaki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Ndullu Tanzania inatakiwa izishukuru sana kampuni za simu kwa hatua hii ambayo imefikiwa, kwa sababu huduma za kawaida za kibenki zilishindwa kukidhi mahitaji ya wengi.

“ Katika mambo ambayo mimi kama Gavana wa Benki Kuu nilisema nitayasimamia kwa dhati lilikuwa ni hili la kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma za kifedha kuliko hali ilivyokuwa. Leo nashukuru hali ni nzuri,” alisema.

Akizungumzia matokeo ya ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Vodacom, Rosalynn Mworia, alisema Vodacom imetiwa nguvu na ukweli kwamba mapinduzi iliyoyaleta katika sekta ya mawasiliano nchini yameanza kuleta matunda.

“Tangu Vodacom imeingia hapa nchini mwaka 2000, imekuwa na kawaida ya kuwa ya kwanza kubuni vitu ambavyo baadaye vimekuwa vikiigwa na wengine. Mfano mmoja wapo wa ubunifu wa Vodacom ni huduma hii ya M Pesa.

“ Hivi sasa hakuna mtu ambaye utakutana naye njiani na umuulize M Pesa ni nini na asijue. Vodacom tunatamka kwa fahari kabisa kwamba sasa tuna wateja zaidi ya milioni tisa ambao wanatumia huduma hii. Hii ni idadi iliyo sawa na taifa kamili katika nchi nyingi duniani,” alisema Mworia.

Kupitia huduma ya M Pesa, wateja wa Vodacom wanaweza kupokea na kutuma fedha kupitia simu zao za mkononi na pia wanaweza kutoa fedha na kuweka katika akaunti zao za benki za kawaida, wakiwa mahali popote ambapo huduma za Vodacom zinapatikana.

Ripoti hiyo ya WB, pamoja na mambo mengine, imeweka bayana mchango mkubwa wa kampuni za simu katika uchumi wa nchi za Afrika, huku ikitamka kwamba kiasi cha fedha kinachozunguka kwa mwaka kupitia huduma kama M Pesa hapa Tanzania kwa sasa ni sawa na asilimia 47 ya Pato la Taifa.

“ Matumizi na imani ya wananchi kwa kampuni za simu imekua sana katika miaka ya karibuni kiasi kwamba watu sasa wanahifadhi zaidi fedha zao katika simu zao za mkononi wakati idadi ya wanaoweka benki fedha zao ikishuka,” ripoti hiyo imebaini.

Vodacom Tanzania ni kampuni tanzu ya kundi la kampuni za Vodacom lenye makazi yake nchini Afrika Kusini. Kampuni hiyo ya Afrika Kusini nayo ni sehemu ya kundi la kampuni za Vodafone lenye makao yake makuu nchini Uingereza.

Chanzo: Swahili Times