SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 13 Agosti 2017

T media news

Fedha za ushahidi wa kesi ya TAKUKURU zaibiwa zikiwa mahakamani

Fedha taslimu Sh200,000 zilizokuwa kielelezo katika kesi ya kuomba na kupokea rushwa inayomkabili ofisa wa polisi wa mkoani Njombe, zimeibwa wakati kesi ikiendelea.

Mbali na fedha hizo, pia hati ya utaifishaji mali (seizure note), ambayo hujazwa wakati wa ukamataji na kusainiwa na mshtakiwa na mashahidi ambayo ni kielelezo, nayo imetoweka.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa vielelezo hivyo muhimu vya upande wa mashtaka ambao ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), vilitoweka Jumatano iliyopita.

Tayari mshtakiwa katika kesi hiyo pamoja na karani mmoja wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi wamehojiwa na polisi mkoani Kilimanjaro, kutokana na kuibwa kwa vielelezo hivyo muhimu.

Imeelezwa kuwa siku hiyo baada ya shahidi wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wake mahakamani, aliomba kupatiwa kielelezo hicho ili akitumie kumuuliza maswali shahidi wa TAKUKURU.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa baada ya kumaliza kukitumia kielelezo hicho, hakukirudisha kwa karani na siku iliyofuata wakati kesi ikiendelea na kielelezo kutakiwa tena, ndipo ilipobainika hakipo.

“Karani alipoulizwa kielelezo akasema hakurudishiwa ile jana yake na ndipo kukawa na kutupiana mpira kati ya karani, mwendesha mashtaka na mshtakiwa,” alidokeza mmoja wa watoa habari wetu.

Chanzo hicho kilidai kuwa, kwa kawaida kielelezo kikishakabidhiwa na kupokewa mahakamani, kinakuwa ni mali ya Mahakama na kinapotumika kwenye ushahidi hurudishwa kwa karani.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, wakati vielelezo hivyo vinatoweka, mashahidi wengine muhimu ambao walishiriki katika ukamataji na wanaotakiwa kuvitumia katika kesi hiyo, walikuwa hawajatoa ushahidi.

Naibu Msajili ya Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Bernard Mpepo alipoulizwa juzi jioni baada ya taarifa hizo kusambaa, alisema hajui lolote kuhusu suala hilo kwa kuwa alikuwa kwenye kikao cha Mahakama ya Rufani jijini Arusha.

Lakini jana, Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Hamis Issah alithibitisha kutoweka kwa vielelezo hivyo na kusema tayari Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi juu wa tukio hilo lisilo la kawaida.

“Inavyoonekana kulifanyika kosa pale mahakamani siku ya kesi. Mshtakiwa aliondoka na vielelezo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ndiyo maana tulimhoji,” alisema.

Polisi huyo alikamatwa Mei mwaka huu na TAKUKURU akidaiwa kupokea 200,000 kutoka kwa mfanyabiashara mmoja aliyekuwa akituhumiwa kukamatwa akiwa na lori linalodaiwa kutumika kusafirisha mahindi ya wizi.

Hata hivyo, alipofika mkoani Kilimanjaro na kumkamata mmiliki wa lori hilo, ilibainika kuwa gari hilo halikuwa la kubeba mizigo, bali la mafuta na halijawahi kutembea tangu linunuliwe.

Pamoja na kubaini tofauti hizo, bado inadaiwa polisi huyo alimweka mahabusu huku akindelea kumtuhumu mmiliki kuhusika na kosa hilo la jinai akisisitiza lazima asafirishwe kwenda Njombe.

Ni katika mazingira hayo, ofisa huyo anadaiwa kuomba kiasi hicho cha fedha ili suala hilo limalizike pasipo mfanyabiashara huyo kuchukuliwa hatua, na ndipo taarifa zilipotolewa TAKUKURU.

Chanzo: Mwananchi