Kwa mujibu wa kura takribani milioni 14 ambazo zimekwisha hesabiwa hadi sasa, Rais wa sasa wa Kenya, Uhuru Kenyatta anaongoza akiwa na asilimia 54.62 huku mpinzani wake mkuu, Raila Odinga akifuatiwa akiwa na asilimia 44.53.
Asilimia 80 ya kura zilizopigwa zimehesabiwa huku Tume ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC) ikitangaza kuwa hadi sasa kura zaidi ya laki 3 zimeharibika kutokana na kukiukwa kwa taratibu za upigaji.
Aidha, Muungano wa NASA ambao ndio wapinzani wakuu wameyakataa matokeo hayo ya awali yanayoonyesha kuwa wapo nyuma kwa asilimia 10 wakidai kuwa kuna nyaraka muhimu zimekosekana kuonyesha uhalali wa matokeo hayo.
Akizungumza, mgombea wa NASA, Raila Odinga amesema kwamba, matokeo hayo yanayotangazwa sasa ni ya kidhahania na kwamba ni batili. Amesisitiza kwamba, taarifa kutoka kwa mawakala wao kwenye vituo vya kupigia kura zinaonyesha kwa yeye (Odinga) ndiye anayeongoza katika mchuano huo.
Kwa upande wake, Tume ya Uchaguzi imewataka raia wote kuwa watulivu na kusubiri matokeo ya mwisho kutangazwa.
Watu wengi wanahofu kuwa huenda machafuko kama ya mwaka 2007 yaliyopelekea vifo vya wakenya zaidi ya 1000 huku zaidi ya 60,000 wakijeruhiwa na wengine kukimbia makazi yao yakatokea tena endapo mmoja kati ya wagombea wawili, Odinga na Kenyatta atakataa kutambua matokeo.