Mbunge wa Kawe na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CHADEMA, Halima Mdee amefunguka kwa kuwapongeza wananchi wa Kenya kwa kuweza kubadilisha Katiba ya nchi yao ambapo leo hii imeweza kuwasaidia wafungwa kupiga kura wakiwa katika magereza yao.
Mdee amebainisha hayo kupitia ukurasa wake twitter baada ya kuona picha zilizokuwa zinagaa katika mitandao ya kijamii asubuhi ya leo zikiwaonyesha baadhi ya wafungwa wa nchi ya Kenya wakiwa wamejipanga foleni wakisubiri kupata haki yao ya msingi ya kupiga kura ya kuchagua viongozi wanaowahitaji.
"Mabadiliko ya Katiba yanavyofanya kazi njema nchini Kenya, Katiba yetu pendekezwa imefungiwa kabatini",ameandika Halima Mdee.
Hata hivyo suala la wafungwa kupiga kura nchini humo ni mara ya kwanza tokea kubadilishwa kwa Katiba yao jambo ambalo limewatamanisha watu wengi kutoka Tanzania nao kutaka wafungwa waliopo kwenye vifungo wapige kura nao katika chaguzi zijazo.
Kwa upande mwingine, Uchaguzi wa mwaka huu unashirikisha wapiga kura takribani milioni 19.6, kukiwa na ongezeko la wapiga kura wapya milioni 5.2 pamoja na kuwepo vituo 40,883 vya kupigia kura na vimefunguliwa tangu saa 12 alfajiri katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo na wanatarajiwa kuhitimisha kupiga kura ifikapo saa 11 alasiri.