Kuna watu bado wana beza mashindano ya Ndondo Cup na kuona hayana tija kwa vijana ambao ndio walengwa hasa ili kuwapa fursa ya kuonekana, lakini wahusika wenyewe wanaheshimu na wanajua thamani yake kwa sababu kupitia mashindano hayo wamefikia angalau nusu ya ndoto zao kwenye soka.
Kutana na Kelvin Sabato ‘Kiduku’ mchezaji wa Majimaji ambaye ametoka kwenye michuano ya Ndondo moja kwa moja na kucheza ligi kuu Tanzania bara kwa mafanikio makubwa.
Mchezaji huyo alikuwepo kwenye mashindano ya msimu wa kwanza kabisa lakini akaendelea kucheza mashindano haya licha ya kwamba alishasogea na kuanza kucheza ligi kuu lakini anasema anacheza Ndondo ili kuwapa hamasa vijana wenzake waliokuwa wakicheza pamoja waone kuwa inawezekana kutoka kupitia Ndondo.
Kiduku amesema hajawahi kucheza kwenye timu rasmi wala mashindano rasmi ya vijana, yeye na Ndondo, Ndondo na yeye hadi amefanikiwa kufika ligi kuu.
“Tangu naanza mpira, sijawahi kucheza Copa Coca-cola, Airtel Rising Stars wala timu ya taifa ya vijana. Mimi nimetokea kwenye Ndondo mpaka ligi kuu,” amesema Kiduku wakati akizungumza na kipindi cha Sports Extra ndani ya Clouds FM.
Huu ni msimu wa nne wa michuano ya Ndondo Cup, Kiduku alikuwa sehemu ya wachezaji walioanza na mashindano haya tangu msimu wa kwanza na ameendelea kuscheza hadi leo.
“Msimu wa kwanza kucheza Ndodo Cup nilikuwa na timu ya Abajalo tukafika fainali na kushinda ubingwa, ukiachana na kucheza mashindano yenyewe lakini unakutana na watu wako wa karibu wengine bado hawajapata nafasi ya kusogea juu kwa hiyo Ndondo inawainua kutoka huko, msimu ambao tulishinda ubingwa tukiwa na Abajalo wapo wengi ambao walipata timu za ligi kuu.”
“Msimu uliofuata nilicheza Ndondo nikiwa Black Six lakini hatukufanya vizuri sana tukatolewa kwenye robo fainali halafu msimu uliopita nikacheza Misosi FC tukafika hadi nusu fainali. Msimu huu nimeamua kurudi nyumbani kuwapa changamoto kwa sababu mimi nimefanikiwa kupitia Ndondo kwa hiyo nataka nikawahamasishe vijana, nitakuwa Stimtosha ipo maeneo ya Mabibo.”
Kiduku anaingia kucheza ligi kuu Tanzania bara
“Baada ya kutoka Abajalo nikasajiliwana Mwadui FC nikapata fursa ya kucheza ligi kuu Tanzania bara kwa mara kwanza.”
“Msimu uliopita nilitoka Mwadui nikaenda Stand United tukapambana pale hadi naondoka Stand timu ilikuwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi. Kilichonifanya nitoke Stand ni kwamba, wakati naingia mimi ndio kipindi timu ilikuwa kwenye mgogoro wadhamini wakaondoka, kwa hiyo kutokana na hali ya maisha nikalazimika kutoka ili kwenda sehemu nyingine kutafuta malisho bora.”
“Niliwaomba viongozi waniandikie barua niondoke kama mchezaji huru, viongozi wakakubali, kwa bahati nzuri nilikuwa kwenye kiwango kizuri kwa sababu ndio nilikuwa nimewapiga Mtibwa hat-trick kwa hiyo nyota ilikuwa inang’aa nikajua sitokosa timu ya kucheza na kupata angalau milioni tatu kwa pamoja kuliko kuendelea kukaa Stand kusubiri milioni 10 ya kidogokidogo.”
“Bahati nzuri Majimaji wakaja kipindi cha dirisha dogo la usajili msimu uliopita nikaenda timu ikiwa chini hadi watu wangu wa karibu walikuwa wananishangaa, lakini mimi nikawaambia ‘mkulima hachagui jembe’, nikaungana na wachezaji wenzangu chini ya Karl Ongala tukainusuru timu kushuka daraja.”
“Nimefunga jumla ya magoli 10 kwenye msimu uliomalizika, nikiwa Stand United nilifunga magoli manne halafu nikafunga magoli sita nikiwa Majimaji.”
Lengo kuu la Ndondo Cup ni kuwatengenezea daraja au jukwaa vijana wa mitaani ambao wana vipaji lakini hawana sehemu ya kuvionesha, kupitia mashindano haya wanapata fursa ya kuonesha vipaji vyao, endapo kuna timu za madaraja ya juu kama ligi daraja la pili, daraja la kwanza na hata ligi kuu zitavutiwa nao, unakuwa mwanzo wao wa kupiga hatua mbele katika safari yao ya soka.