Katibu Mkuu wa wizara ya maji na umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo amewakejeli watu wanaopinga ripoti mbili za mchanga zilizowasilishwa na tume mbili tofauti za wasomi kwa Rais John Magufuli.
Profesa Kitila ambaye alikuwa mshauri wa chama cha ACT-Wazalendo, ametumia mtandao wake wa Twitter kufikisha ujumbe wake kwa watu aliodai wanapinga kila kitu.
“Kuna ugonjwa unaitwa opposition defiant disorder (ODD). Dalili kubwa ni kupinga kwa lengo la kupinga hadi unajipanga mwenyewe. Tuuepuke!,”aliandika Profesa Mkumbo.
Mkumbo aliandika wazo hilo baada ya kuwepo baadhi ya watu walioonekana kupinga ripoti na maamuzi ya kamati iliyoongozwa na Profesa, Nehemiah Osoro.
Hata hivyo, watanzania wengi ikiwa ni pamoja na wasomi wameonesha kuunga mkono ripoti hiyo na mapendekezo yote yaliwasilishwa, ambayo Rais John Magufuli aliahidi kuyafanyia kazi yote.