Salum Mayanga kocha mkuu wa kikosi cha Stars hakubaliani kabisa na wanaosema au kudhani kwamba, timu ya taifa ya Lesotho ni ‘kibonde,’ Mayanga anaami kuwa kwenye mashindano hakuna timu kibonde.
Mayanga anachoamini yeye ni kwamba Stars ilishindwa kuibuka na ushindi dhidi ya Lesotho baada ya kuruhusu goli rahisi la kusawazisha na badae kubanwa na kushindwa kutengeneza nafasi za kutosha kuongeza magoli mengine.
“Kwanza lazima tukubali kwenye mashindano hakuna timu ‘kibonde’ lakini tulitangulia kufunga goli, leo tumecheza mchezo wa kushambulia tukiwa na washambuliaji watatu ndio ulikuwa mpango wetu lakini tumefanya makosa tumeruhusu goli rahisi la kusawazisha.”
“Matokeo ya sare kwa nyumbani si mazuri lakini ndio matokeo ya mchezo yaliyotokea kwa siku ya leo, tulianza game vizuri kwa kutangulia kufunga goli kwa bahati mbaya hatukuwa makini tukawapa nafasi kirahisi wakaweza kusawazisha goli baada ya hapo walitengeneza ulinzi wa kutosha ikatupa wakati mgumu wa kuweza kutengeneza nafasi kufunga goli la pilina kuongoza la tatu.”
“Kwa upande wangu ni changamoto kosa lililojitokeza la kuruhusu goli lirudi nadhani tutapata muda wa kufanya marekebisho na kuona mechi zinazofuata tunafanya vizuri zaidi.”
“Baada ya wao kupata goli la kusawazisha, wakafunga eneo lao la nyuma ikawa kasi sisi kupata nafasi ya kufunga goli lingine.”
Maynaga pia amesema, kushindwa kupata matokeo ya ushindi kwenye mechi dhidi ya Lesotho si kwamba ndio mwisho wa safari ya Stars kufuzu kwenda kucheza fainali za AFCON .
“Bado tutaendelea kufanya mazoezi na kurekebisha makosa tuliyofanya ili michezo inayokuja tuone nini kitatokea.”