Dkt. Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga akizungumza na mwandishi wa gazeti la Mwananchi alisema yupo tayari kuhojiwa na vyombo vitavyomhitaji.
Dkt. Peter Kafumu
Dkt. Kafumu amesema hayo baada ya jana Rais Dkt. Magufuli kusema kuwa Dkt. Kafumu alikuwa anafanya kila jitihada kukutana na kumshawishi Mwenyekiti wa Kamati ya Kwanza ya Kuchunguza Mchanga wa Madini, Profesa Mruma abadili baadhi ya vipengele katika ripoti yake aliyoiwasilisha kwa Rais na kwamba anashangaa kwa nini msomi huyo amekosa aibu na uzalendo na kukubali kutumiwa.
“Nisingependa kuzungumza lolote kuhusu mapendekezo hayo, nitakuwa nazungumza kabla ya kuhojiwa na Serikali kwani ni mmoja kati ya waliotajwa. Nitakuwa tayari kuhojiwa kwa sababu ni maagizo ya Rais,” alisema Dkt. Kafumu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja alisema hawezi kuzungumzia agizo la Rais Magufuli la kuhojiwa na vyombo vya usalama kutokana na kuhusika kwake katika mikataba ya madini. Hata hivyo alitaja uzembe wa usimamizi wa Sheria kwakuwa ndiyo uliolifikisha Taifa hapa kwakuwa Sheria zilizopo ni nzuri lakini hazisimamiwi ipasavyo.
Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja
“Kuhusu kuhojiwa au kuwajibika sina neno la kusema lakini nampongeza sana kwa moyo wa dhati Mheshimiwa Rais maana amezungumza kwa hisia na uzalendo kabisa kuhusu tunachostahili kupata badala ya tunachopata,” alisema Ngeleja.
Hata hivyo, alikiri kuwa mikataba mingi iliyopitishwa siyo mizuri kwakuwa inawanyonya Watanzania ambao wameshindwa kupitia Sheria mpya (ya madini ya mwaka 2010) kuifanyia kazi.
“Kifungu cha 11 pia kinachosema mikataba yote ipelekwe Bungeni baada ya miaka mitano na kifungu cha 10 kinasema Serikali ishiriki kimkakati kwenye migodi, lakini usimamizi wake ndiyo shida,” aliongeza.
Kuhusu mchanga kusafirishwa nje ya nchi, alisema walishaliona jambo hilo mapema lakini wakabainisha kuwa mashine za kufanya kazi hiyo zina gharama kubwa zaidi hivyo kuhitaji ubia katika ujenzi baina ya Serikali na sekta binafsi.
Chenge hakutaka kuzungumza na waandishi wa habari waliomfuata mara baada ya kuahirishwa kikao cha Bunge jana. “Siongei na watu,” ndiyo maneno pekee aliyoyasema Mbunge huyo wa jimbo la Bariadi Magharibi.
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge
Baada ya kupokea ripoti ya Kamati Pili ya Uchunguzi wa mchanga wa madini, Rais Magufuli aliagiza Mawaziri wote wa Nishati na Madini waliohusika kwenye mikataba ya uchimbaji madini, manaibu wao, waliokuwa wanasheria wakuu wa serikali wote, watendaji wao pamoja wa kila aliyehusika aitwe na vyombo husika na kuhojiwa.