Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffar Michael
Moshi. Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffar Michael na Meya wa Mji wa Moshi, Raymond Mboya wameeleza namna walivyozuiwa kuingia Ikulu ya mjini Moshi kuzungumza na Rais John Magufuli.
Viongozi hao ambao wanatokana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walikumbana na kadhia hiyo saa 6:00 mchana wakati wakiwa katika foleni ya ukaguzi wa maofisa usalama.
Mbunge Michael alisema aliamriwa kuondoka akiwa katika foleni Ikulu, lakini akasema awali alijulishwa na Meya Mboya kuwa walihitajika katika kikao hicho.
“Ni kweli nikiwa kwenye foleni alikuja ofisa usalama mmoja akaniambia kistaarabu tu kuwa mimi sikuwa natakiwa nilijaribu kumwambia mimi ni Mbunge lakini akasisitiza siruhusiwi,” alisema Mbunge huyo.
Mstahiki Meya Mboya alisema alijulishwa na viongozi wa halmashauri na ofisi ya mkuu wa mkoa kuwa wangehitajika.
“Niliambiwa Mkurugenzi wangu alifanya mawasiliano na Ras (Katibu Tawala wa mkoa) na wote wakaona ipo haja ya sisi kama wenye mji kuwapo lakini ndio hivyo tulizuiwa,” alisema.