SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 3 Mei 2017

T media news

MAGUFULI Ampa Tano Dk Mengi kwa Uwekezaji Nchini..!!!


RAIS John Magufuli amempongeza Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Regnald Mengi kwa kufanya uwekezaji wa Kiwanda cha Kutengeneza Vinywaji Baridi Jamii ya Coca Cola cha Bonite Bottlers Limited (BBL) cha Moshi mkoani Kilimanjaro.

“Nimemuona Dk. Mengi yuko pale na kwa kweli naomba nimpongeze kwa kile Kiwanda chake cha Bonite alivyowekeza, hongera sana. Wazawa wengine wa Kilimanjaro rudini nyumbani muwekeze. Huyu Dk. Mengi anapiga kote kote Dar na Moshi,”alisema.

Rais Magufuli alitoa pongezi hizo  wakati wa sherehe za maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi duniani (Mei mosi) zilizofanyika kitaifa mjini Moshi kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Pongezi hizo za Rais, ziliamsha hisia za furaha za maelfu ya wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro waliofurika katika sherehe hizo na kumshangilia Dk. Mengi, baada ya Rais Magufuli kumsimamisha na kumtaka awapungie mkono.

Dk. Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) amekuwa akisisitiza suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi kuwa ni njia pekee duniani iliyoonesha mafanikio katika kukuza uchumi wa nchi mbalimbali,kupunguza umaskini na kudumisha amani na utulivu.