Hatimaye kivuko kipya cha MV KAZI kimefanyiwa majaribio ya kubeba abiria na magari kwa mara ya kwanza Jijini Dar es Salaam baada ya kukamilika kwa matengenezo yake.
Majaribio hayo yalifanyika kulingana na sheria na taratibu za vyombo vya majini ambayo inavitaka vyombo vyote vya majini kufanyiwa majaribio kabla ya kuanza kazi ili viweze kupatiwa cheti cha ubora “Seaworthiness Certificate”.
Awali wataalam kutoka Chuo cha Ubaharia Dar es Salaam (DMI) waliweza kupima ubora na uimara wa kivuko hicho kwa kutumia utaratibu wa kuweka mawe yenye kilo zinazolingana na uwezo wa kivuko pamoja na magunia ya mchanga ili kuweza kupima uwezo wa kivuko kulingana na mahitaji yaliyoainishwa kabla hakijabeba abiria na mizigo.
Zoezi hili pia lilihusu kufanyika kwa kipimo cha kuhakikisha kuwa kivuko hakilali upande mmoja yaani “Inclination test” ambapo kilionyesha Kivuko kiko sawa. Taarifa ya zoezi hili itakuwa sehemu ya vitu vya makabidhiano wakati wa upokeaji wa Kivuko.
Ujenzi wa MV KAZI umegharimu Shilingi Bilioni 7.3 za Kitanzania na kina uwezo wa kubeba abiria 800 magari 22 sawa na jumla ya tani 170. Kivuko hicho kitakabidhiwa rasmi hivi karibuni kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa ajili ya kuanza kutoa huduma kati ya Magogoni na Kigamboni Jijini Dar es salaam na kuongeza idadi ya vivuko katika eneo hilo kufikia vitatu.
Kivuko cha MV KAZI kikiondoka kwa mara ya kwanza kutokea Magogoni kuelekea Kigamboni kikiwa na abiria na magari. Kivuko hicho kilikua kikifanyiwa majaribio mara baada ya ujenzi wake kukamilika kabla ya kukabidhiwa kwa TEMESA.
Abiria wakiingia katika kivuko cha MV KAZI tayari kwa kuvuka kuelekea upande wa Kigamboni. Kivuko hicho kilikua kikifanyiwa majaribio ya kubeba abiria kwa mara ya kwanza baada ya ujenzi wake kukamilika hivi karibuni.