Unakupokuwa na uhusiano na mtu, kila mmoja anatamani ifike siku wote wawili muweze kuishi pamoja, lakini siku hiyo huwa haiji hivi hivi, kuna hatua mnatakiwa kupitia tena kwa uwazi kufika hapo.
Moja ya hatua kubwa ambazo zinawatatiza watu wengi ni kuwapeleka wenza wao kuwatambulisha nyumbani kwani hakika hilo huwa ni zoezi gumu. Suala hili hutofautiana kulingana na jamii ambazo wahusika wanatoka. Kwa upande wa jamii za Kiafrika mfano Tanzania, kwenda kumtambulisha mchumba sio kazi rahisi.
Changamoto kubwa inayowakumba watu wengi ni namna ya kufahamu jinsi ya kufanya utambulisho huo lakini pia kufahamu wakati sahihi wa kufanya hivyo.
Unaweza ukatamani uwekwe kwenye chumba uulizwe maswali ya kila namna kana kwamba unaomba kazi kuliko kutakiwa kumtambulisha mchumba kwa wazazi.
Licha ya kuwa huenda mchumba wako alikuwa akija kwenu na mnakaa mnazungumza, lakini unapofika wakati wa kwenda kumtambulisha rasmi, changamoto huwa ni kubwa.
Kuna vitu vya msingi, kote kwa mwanaume na mwanamke vya kuzingatia kabla ya kwenda kumtambulisha mchumba wako unayetaka muoane kwa wazazi wako
Hakikisha unauhakika na huyo unayetaka kwenda kumtambulisha. Kabla ya kufanya maamuzi haya magumu katika maisha, kuwa na uhakika naye, itambue nafasi yake katika maisha yako, mtambue yeye ni nani na anaweza kuwa nani, jiulize maswali mengi kadiri uwezavyo na ukiona yote yanapata majibu pasi na ukakasi, basi huyo anakufaa.
Tambua kuwa unachagua mtu wa kwenda kuishi nae maisha yako yote yaliyobaki na sio mtu utakayemuacha baada ya miezi miwili, hivyo mchunguze, mfahamu uridhika naye.
Mfahamishe mpenzi wako kuhusu historia na nyakati mbalimbali katika familia yako. Maelezo hayo siyo lazima yawe ya kina sana kwani mtaendelea kufahamiana kadiri siku zinavyozidi kwenda, lakini nilazima aelewe kuhusu familia yake.
Jaribu kufikiri umempelea mpenzi wako kwenye halafu anamuuliza baba yake, sikukuu ya Christmass ilikuwaje? wakati kipindi cha sikukuu hiyo baba yako alikuwa anaumwa mahututi.
Ili kuepuka mambo kama hayo ni vizuri mkawa mnafahamiana vizuri ili akiwa na wazazi pamoja na ndugu zako mjue nini cha kuzungumza na nini si chakuzungumza.
Jambo jingine hakikisha anakuwa tayari kwenda kuonana na wazazi wako, msifanye kulazimisha au kupelekena mapema nyumbani. Mapenzi huwa ya mambo mengi sana, lakini umjue mkigombana anakuwaje ili muweze kuyakabili hayo kwenye ndoa.
Mapenzi mwanzoni huwa ni matamu sana na yenye kujaa upendo, chunga hayo yasikuhadae ukaenda kumtambulisha mpenzi wako na kufunga ndoa haraka haraka, hakikisha umeijua kila tabia yake ndio ufanye hivyo.
Hivyo ni baadhi ya vitu vingi unavyotakiwa kuvifanya au kuzingatia kabla ya kumtambulisha mchumba wako. Kuna mambo mengine kama kujichunguza kama upo tayari kwa ndoa, kuzijua afya zenu, kujua historia za familia kiundani.