Makamu wa Rais wa klabu ya Simba Geoffrey Nyange Kaburu amesema, uongozi wa klabu hiyo haukukurupuka kusaini mkataba na SportPesa kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.
Baada ya MO kudai alipwe gharama zote alizokuwa akiisaidia klabu ya Simba kutokana na klabu hiyo kusaini mkataba wa udhamini bila kumshirikisha, baadhi ya wadau wamekuwa wakiukosoa uongozi wa Simba kwamba ulikurupuka kusaini mkataba huo bila kumshirisha MO.
“Uongozi wa Simba haukukurupuka kusaini mkataba na SportPesa, unajua nini ambacho unajifanya, unafahamu mahitaji ya Simba na faida ya wadau wetu wengine wawekezaji wa badae kama MO.”
“Kuna mambo mengi ambayo siwezi kuyasema hapa kwa sababu yataathiri mazungumzo yetu na MO, kwa hiyo itakua busara kama tukiacha kwanza hadi pale tutakapozungumza na MO na baada ya hapo nadhani tutakuwa na kitu kizuri cha kuongea kwa maslahi ya klabu ya Simba.”
Siku moja baada ya uongozi wa Simba kusaini mkataba wa udhamini na kampuni ya SportPesa, MO aliibuka na kutaka Simba imlipe gharama zote ambazo alikua akiisaidia kama makubaliano yao yalivyokua wakati wakielekea kwenye mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu hiyo.