Na Baraka Mbolembole
INAWEZEKANA ni kweli mlinzi wa kati wa Kagera Sugar FC, Mohamed Fakhi alicheza mchezo wa Kagera 2-1 Simba SC akiwa na kadi tatu za njano, lakini Shirikisho la Soka nchini-TFF wamewapa Simba barua inayoonesha mchezaji huyo hakuwa na kadi tatu za njano-ambazo Simba wanadai ilikuwa hivyo.
MALALAMIKO YASIYO NA MASHIKO FIFA
Simba wamepeleka malalamiko yao FIFA wakiwa na nakala ya barua kutoka TFF ambayo wanadai haikuwatendea haki. Ieleweke Simba wameenda FIFA wakiwa na barua ambayo inaonyesha ‘mchezaji anayelalamikiwa’ hakuwa na kadi tatu za njano.
Kwa hiyo wanachojaribu kufanya viongozi wa Simba hivi sasa ni kuendelea kuwahadaa wanachama wao kwa sababu makosa ni yao wenyewe. Inawezekana makosa yasiwe yale ya kupoteza mchezo wa Kagera sababu bahati nzuri hawajanyang’anywa ushindi wao, bali wanapigania ushindi ambao hawakuupata ndani ya dakika 90.
Kama unaona mbali katika hili unaweza kuona malalamiko ya Simba waliyopeleka FIFA hayana ‘mashiko,’ na nachokiona ni muendelezo wa utawala kutafuta mahala pa kufichia makosa yao. FIFA haiwezi kutengua chochote katika ligi kuu ya Tanzania Bara na hata watakapoulizia suala hilo kwa TFF watajibiwa kama walivyoambiwa Simba-Fakh hakucheza Kagera 2-1 Simba akiwa na kadi tatu za njano. Mwisho.
Unadhani FIFA wataamua lolote bila kuwashirikisha TFF? Labda watajaribu kuomba kumbukumbu tu za mchezaji lalamikiwa-ambazo kimsingi hazipo na zilizopo zinamruhusu Faskhi kucheza mchezo aliocheza dhidi ya Simba.
Je, hizo kumbukumbu zipo? Kwa sisi ambao hatujaona hatuwezi kusema sana lakini tayari wale ambao waliona na kuhusika katika mchezo wa Kagera vs African Lyon hadi kwa wale waliosimamia mchezo huo wanasema ‘hakukuwa na kadi yoyote iliyotolewa na mwamuzi katika mchezo huo.’
‘Barua ya Simba SC kwenda FIFA ni anguko lao lingine, watashindwa kwa sababu barua ya TFF ilisema wazi kuwa Fakhi hakuwa na kadi tatu za njano wakati alipoichezea Kagera dhidi yao. Kama walidhamilia kushinda ‘ubingwa wa mezani’ Simba walipaswa kuvuta subira.
Baada ya katibu mkuu wa TFF kusema mbele ya vyombo vya habari kuwa Fakhi aligundulika kuwa na kadi tatu za njano ila Simba hawatapewa pointi baada ya kuwasilisha malalamiko yao nje ya muda tena bila malipo ya ada ya malalamiko, wao wangesubiri barua rasmi kisha wangeenda FIFA ambako wangepata haki yao.
Lakini kitendo cha ‘kukurupuka’ na kusema wanaenda Fifa kudai haki yao kiliwastua TFF na kuona njia sahihi ya kuwamaliza ni kuwapa barua inayosema Fakhi hakuwa na kadi tatu za njano siku anacheza dhidi yao. Hawana busara na ustahimilivu. Mchezo umeishia hapo.
FIFA husisitiza kuhusu ‘mchezo wa kiungwana’ katika soka na hawapendezwi na mabingwa wanaotokana na pointi za mezani hivyo si rahisi kuona Simba ikishinda ubingwa wa VPL kwa msaada wa ‘meza za FIFA’ baada ya kushindwa uwanjani. Naamini hilo na Yanga ndiyo mabingwa stahili wa VPL msimu wa 2016/17.
LICHA YA KUSHINDWA KUBEBA VPL, SIMBA IMEPIGA HATUA
Kuna sehemu ambazo Simba wameonekana kufanikiwa, lakini bila uwepo wa busara na hekima hata zile sehemu walizofanikiwa msimu uliomalizika wataporomoka tena kama viongozi hawatabadilika.
Mfano sehemu ya timu, ndani ya uwanja Simba wamefanikiwa kuwakusanya wachezaji wengi bora vijana raia wa Tanzania na ni hawa ambao wameisaidia Simba kupanda hadi nafasi ya pili katika ligi baada ya kumaliza nafasi ya nne msimu wa 2012/13 na 2013/14.
Walimaliza nafasi ya tatu mara mbili misimu ya 2014/15 na 2015/16 hivyo kitendo cha kumaliza nafasi ya pili msimu huu huku wakisubiri mchezo wa fainali ya FA Cup ni wazi hayo ni mafanikio makubwa kwao licha ya kutoshinda ubingwa.
Ili kushinda ubingwa wao wa kwanza Simba wanapaswa kujipanga zaidi na kusahihisha makosa yaliyowaangusha kwa misimu mitano iliyopita lakini hilo kwao ni gumu kwa sababu wanaachana na sababu za kweli na kudili na sababu za uongo kama ndizo huchangia kuanguka kwao.
KWANINI SIMBA WANAFELI KILA MSIMU?
Msimu huu uliomalizika Jumamosi iliyopita ilionekana kama vile Simba wangefanikiwa kushinda ubingwa lakini mwishoni wameshindwa kwa tofauti ya magoli tu na ‘watani’ wao wa jadi Yanga SC. Kwa jicho langu la tatu naona sababu iliyowaangusha ni ukosefu wa busara na hekima miongoni mwa viongozi-tena ni wawili au watatu tu ambao wapo pale.
Kama wataamua kufanya mambo kwa hekima na busara wanaweza kufanikiwa lakini kwa hali jinsi ilivyo si rahisi kwao kushinda hata mchezo wa fainali dhidi ya Mbao FC katika fainali ya FA siku ya Jumamosi ijayo. Simba atapoteza mchezo ujao kwa sababu ndani yao wenyewe wanatengeneza ‘hujuma’ ili timu isifanikiwe kwa maslahi ya watu wachache.