Baada ya kuandamwa na matokeo mabovu kwa muda mrefu, hatimaye Sunderland wameshuka daraja kwa mara ya nne katika ligi kuu ya Uingereza Epl.
Sunderland walikuwa uwanja wao wa nyumbani wa Stadium of Light wakati wakiikaribisha timu ya Fc Bournemouth na mashabiki wao waliamini wanaweza pata matokeo katika mchezo huo.
Alikuwa Joshua King aliyeweka machozi kwenye mashavu ya mashabiki wa Sunderland kwani bao lake dakika ya 88 liliwaonesha Sunderland mlango wa kutokea Epl.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Sunderland David Moyes alisema hana mpango wa kuondoka katika klabu hiyo bali anataka kupambana ili kuirudisha tena ligi kuu.
“Sunderland watapambana tena na nina uhakika katika hilo, kwa sasa inatupasa kuwa kitu kimoja kuanza kuweka mipango yetu pamoja ili turudi tena msimu ujao” alisema Moyes
Katika michezo mingine goli la Jamie Vardy aliwapa ushindi Leicester dhidi ya Westbrom, Southampton na Hull City wakatoka suluhu ya bila kufungana kama ilivyo kwa Stoke City na West Ham.