AMEPONYOKA! Matumaini ya baadhi ya watu kuwa arobaini ya sakata la kigogo anayedaiwa kutumia cheti cha mtu mwingine kuwa imewadia, yameyeyuka.
Matumaini hayo yalitoweka baada ya kigogo huyo anayedaiwa kujiendeleza kielimu kwa jina la mtu mwingine na kuachana na matokeo mabovu ya kitaaluma yatokanayo na jina lake halisi la Bashite kutoguswa katika ripoti ya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma.
Aidha, maswali mapya yanayodaiwa kuibuka sasa kuhusiana na hatima ya sakata la Bashite ni pamoja na nia ya baadhi ya kutaka kujua suala hilo litashughulikiwa vipi kwa sasa baada ya ripoti iliyowasilishwa jana kwa Rais John Magufuli kutotoa majibu.
Hivi karibuni, sakata la Bashite lilitikisa katika vyombo mbalimbali vya habari hadi kutungiwa nyimbo. Baadhi ya wabunge katika vikao vya Bunge la Bajeti vinavyoendelea mjini Dodoma waliibua pia jambo hilo, wakitaka Serikali itoe ufafanuzi kutokana na kuwapo kwa tuhuma kuwa mmoja wa wateule wa Rais John Magufuli kwa nafasi za ukuu wa mikoa alitumia vyeti vya mtu mwingine kujiendeleza kielimu na kuachana na jina lake la Bashite.
Katika ufafanuzi ulioonekana kutotoa hatima ya kuhusu suala la Bashite, Serikali ilisema uhakiki wa vyeti uliofanyika kwa watumishi wa umma nchini kote haukuhusisha viongozi wa kisiasa.
Akizungumza kabla ya kukabidhi ripoti hiyo kwa Rais Magufuli wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), mjini Dodoma jana, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema kazi ya uhakiki haikuwagusa viongozi wa kisiasa wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wabunge na madiwani bali watendaji pekee wakiwamo makatibu wakuu, walimu pamoja na watumishi wengine wasio na vyeo vya kisiasa.
“Uhakiki huu hauwahusu viongozi wenye vyeo vya kisiasa kama Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Madiwani,” alisema Kairuki.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, uhakiki ulihusisha vyeti vya watumishi zaidi ya 400,000 na kati ya hivyo, 9,932 vilibainika kuwa ni vya kufoji, sawa na asilimia 2.4.
Vyeti vingine vya majina zaidi ya 15,00 vilibainika kutumiwa na watumishi zaidi ya mtumishi mmoja na watumishi 11,596 walibainika kuwa na vyeti vya kitaaluma pekee bila ya vile vya kidato cha nne na sita.
Aidha, vyeti vya watumishi 376,969 (asilimia 94.2) vikionekana kuwa halali na havina shaka.
WABUNGE WANENA
Wakizungumza na Nipashe kuhusiana na suala la Bashite, baadhi ya wabunge walisema kiitaratibu, uhakiki uliofanyika usingeweza kugusa viongozi wa kisiasa kama Waziri Kairuki alivyosema na hivyo, kazi iliyobaki ni kutumia njia nyingine za kusaka ukweli wa jambo hilo.
“Ni kweli kwamba viongozi wa kisiasa hawabanwi sana kuhusu suala la vyeti vya kitaaluma, lakini linapokuja suala la mtu kutumia cheti cha mtu mwingine, ni wazi kwamba hapo kuna kughushi… na hilo ni kosa kubwa linaloweza kumfunga mtu jela. Hivyo suala la Bashite linapaswa kufanyiwa kazi zaidi.
Hatutaacha kulifuatilia,” mmoja wa wabunge wa kambi ya upinzani aliiambia Nipashe jana.
Mbunge mwingine aliyekataa jina lake kutajwa aliipongeza serikali kwa uhakiki uliofanyika kwa sababu utatoa fursa za ajira kwa vijana wenye sifa ili wazibe nafasi zitakazoachwa na pia kukomesha vitendo vya udanganyifu katika elimu.
“Hata hivyo, hili suala la Bashite linapaswa pia kutolewa ufafanuzi wa kina. Ni kwa sababu linahusisha uvunjifu wa sheria na kwa utaratibu wetu hakuna mtu aliye juu ya sheria. Serikali inapaswa kutoa ufafanuzi wa kina ili kumsafisha anayetuhumiwa au kumchukulia hatua,” mbunge mwingine aliongeza.
Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara, akizungumza baada ya uamuzi huo, alisema anaipongeza serikali kwa mcakato mzima walioufanya kuhusu kuwafurumusha watumishi hewa na wale wenye vyeti vya kughushi.
Waitara alisema ilichofanya serikali ni kitu cha kupongezwa, lakini hawezi kukubaliana na kutowahusisha viongozi wa kisiasa ambao baadhi yao wanatuhumiwa kutumia majina bandia wakiwamo wakuu wa mikoa.
“Naungana na serikali kwa mchakato mzima walioufanya hata kuwabaini watumishi hewa pamoja na wenye vyeti ‘feki’, lakini wapo wakuu wa mikoa wanaotuhumiwa kutumia majina ambayo si yao, wameachwa,” alisema Waitara.
Alisema mkuu wa mkoa mmoja katika mji mkubwa, anatuhumiwa kutumia majina ambayo si yake, lakini amekingiwa kifua kwa madai uhakiki hauwahusu wanasiasa, anapingana na hilo.
Waitara alisema kuachwa kwa Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Madiwani, kunajenga matabaka na chuki kati yao na watumishi waengine wa umma.
“Kama Mkuu wa Mkoa anatuhumiwa kaghusi vyeti na kutumia majina ambayo si yake, sasa akiitwa awe mgeni rasmi kwenye mahafali ya chuo, atazungumza kitu gani mbele ya maprofesa….jambo hilo liangaliwe,” alisema.
Alisema uhakiki haupaswi kubagua viongozi kwa sababu wote wanawajibika katika tume ya maadili ya umma, hivyo kuwaacha wakuu wa mikoa na viongozi wengine wa kisiasa, kunataleta mtafaruku.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema uhakiki huo ulipaswa kuzingatia malalamiko ya wananchi kwa kuhusisha pia wanasiasa..
“Hiyo ni double stanbard. Ni vizuri kama malalamiko ya wananchi yangetazamwa na kuhusisha sisi wanasiasa katika uhakiki,” alisema Zitto.