Staa wa filamu Bongo, Wema Sepetu anatajwa kuhusika na majanga yanayomkumba Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda kufuatia yale ambayo amekuwa akiyafanya tangu atajwe kwenye listi ya wanaotumia madawa ya kulevya.
Makonda tangu ajiingize kwenye vita dhidi ya madawa ya kulevya, amekumbana na changamoto nyingi ikiwepo kuibuliwa kwa madai kuwa vyeti vyake vina walakini na ‘kung’ang’aniwa’ na jamii ya waandishi wa habari baada ya kuvamia katika Studio za Clouds Media akiwa na askari wenye silaha.
Majanga haya yanadaiwa kuwafanya wale wabaya wake kuchekelea huku Wema akitajwa kuwa mmoja wao.
KIVIPI?
Wema alitajwa kwenye listi hiyo Februari 2, mwaka huu na kutakiwa kuripoti kwenye Kituo Kikuu cha Polisi ‘Sentro’ wakiwemo mastaa wengine ambapo yeye alionekana kutofurahishwa na kitendo hicho hivyo ikadaiwa kuwa, manung’uniko yake huenda yamechangia Makonda kuandamwa na majanga.
TASBIHI YAHUSISHWA
Aidha, mara baada ya Wema kutajwa kwenye listi hiyo kisha soo kwenda polisi na hatimaye kupandishwa kizimbani, mdada huyo mara kadhaa anapokwenda mahakamani amekuwa na kitu kinachoitwa tasbihi (angalia picha ndogo ya Wema ukurasa wa mbele sehemu iliyozungushiwa) ambacho kinatajwa kuwa na nguvu ya kumuweka mtu mbali na matatizo lakini pia kwa wale wenye nia ya kutaka upatwe na majanga, yanaweza kuwarudia.
TASBIHI NI NINI?
Hiki ni kifaa chenye vitu vya mviringo vilivyochomekwa kwenye uzi ambacho Waislam hukitumia kwenye kufanyia ibada. Akizungumza na Ijumaa, ustaadhi mmoja aliyeomba jina lake lisitajwe gazetini alisema kuwa, tasbihi inapoombewa kisha ukawa unatembea nayo na kuitumia kiibada, inao uwezo wa kukuepusha na mabalaa lakini pia inao uwezo wa kuwafanya wanaokuombea mabaya, yawarudie.
“Unajua haya mambo ni ya kiimani sana, tasbihi kiimani ina nguvu kubwa kama utaitumia vizuri, wapo mashehe wanaoweza kuisomea ile kisha ukapewa na ukawa unatembea nayo, kama umeiva kiimani mabaya hayawezi kukupata lakini wabaya wako yatawafika kwa uwezo wa Mungu,” alisema ustaadhi huyo.
WEMA NA MAKONDA
Licha ya maelezo hayo, baadhi ya watu kwenye mitandao mbalimbali wamekuwa wakidai kuwa, huenda lile chozi la Wema na watu walio nyuma yake lina nafasi kwenye haya mabalaa yanayompata Makonda licha ya kwamba huenda yametokea kwa mipango ya Mungu tu.
“Wema lazima huko aliko atakuwa anafurahia yanayomkuta Makonda, inawezekana kweli anatumia hayo madawa ya kulevya kama ilivyodaiwa lakini huenda kwa yeye ambaye amekuwa nao karibu sana alitaka busara itumike kwenye kumtaja.
“Yawezekana nia ya Makonda ilikuwa njema ya kumtaka kumsaidia Wema aondokane na tatizo hilo lakini ‘approach’ iliyotumika ni wazi haikumfurahisha na ndiyo maana inawezekana sana na yeye alikuwa akiombea yamfike kiongozi huyo,” alidai Husna Juma, mkazi wa Sinza, Dar.
KISOMO NACHO CHAHUSISHWA
Aidha, wapo waliounganisha yanayomkuta Makonda sasa hivi na kisomo alichokifanya Wema nyumbani kwa mama yake, Sinza jijini Dar ambacho nacho kiimani kinatajwa kuwa kina nguvu ya kumfanya anayeombewa kuepushwa na shari na wanaomuombea shari, iwarudie.
USAHIHI
Hata hivyo, usahihi kamili ni kwamba unapofanya kisomo lengo ni kumuomba Mungu akujaalie kila la kheri na kukuepushia kila shari lakini huwezi kuomba maaalum ili kumuombea f’lani mabaya. Kwa maana hiyo wanaodhani kisomo alichofanya Wema K inahusika moja kwa moja kwenye majanga yanayompata Makonda watakuwa wanakosea.
WEMA ANASEMAJE?
Ijumaa lilifanya jitihada za kumpata Wema ili kuzungumzia madai kwamba sononeko lake linahusika katika haya yanayompata Makonda lakini simu yake iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa SMS, hakujibu.
Hata hivyo, kuonesha kuwa hamfagilii Makonda bali yuko upande wa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, staa huyo ambaye hivi karibuni alijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alitupia kwenye ukurasa wake wa Instagram picha ya Gwajima kisha kuweka maneno yaliyosomeka:
“Huyu ni kati ya wanaume ninaowapenda kwa sasa.”