MKATABA WA JEBA NA MTIBWA UNAISHA MSIMU HUU MWEZI WA 5, VILABU VYENGINE TAYARI KUMTOLEA MACHO
Na Abubakar Khatib ‘Kisandu’, Zanzibar
Mkataba wa kiungo wa Mtibwa Sugar, Ibrahim Rajab ‘Jeba’ unaisha mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara na tayari baadhi ya vilabu vimeshaanza kuonesha kuhitaji saini yake.
Jeba kwa sasa hana tena mpango wa kubaki Mtibwa timu ambayo amechezea kwa misimu mitatu mfululizo akitokea timu ya Chuoni kwenye ligi kuu soka Visiwani Zanzibar ambapo pia bado anamatumaini ya kurejea kucheza timu hiyo ya Chuoni ambayo amekiri kuizimia.
Jeba amesema mkataba wake unaisha mwezi Mei na yupo tayari kwenda kucheza popote endapo watafikia makubaliano ambapo mpaka sasa kuna vilabu tayari vimeshaanza mazungumzo na kiungo huyo.
“Ni kweli Kisandu mkataba wangu unaisha mwezi Mei mwaka huu na sifikirii kubaki tena Mtibwa, nataka kubadilisha upepo maana Mtibwa nimeshadumu miaka 3 sasa, kuna baadhi ya vilabu vimeonesha nia ya kunihitaji na pia nasubiri mazungumzo zaidi, lakini pia nafikiria kurejea nyumbani Zenj kuichezea timu yangu ya zamani Chuoni,” alisema Jeba.
Januari 10, 2016 Jeba alizidi kupata umaarufu baada ya kuwafunga na kuwatesa Simba katika mchezo wa nusu fainali Mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambapo Mtibwa Sugar iliichapa Simba 1-0 kwa bao safi la Jeba katika dakika ya 45 baada ya Shiza Kichuya kupiga shuti kali lililomfanya Peter Manyika kutema na Ibrahim Jeba kupachika goli la ushindi.
Jeba ni kipenzi cha mashabiki wa soka Tanzania bara mpaka Visiwani Zanzibar hasa hasa maeneo ya Magomeni Mjini Unguja ambapo ndio nyumbani kwao kiungo huyo huku wachezaji wengi vijana wakitamani kuwa kama kiungo huyo.