SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 29 Machi 2017

T media news

Vita vya Madawa ya Kulevya Vyaamia kwa Mawakili wa Serikali ya Rais Magufuli,Huu Ndio Mchezo Wanaoufanya Kupiga Pesa Ndefu Kupitia Madawa ya Kulevya ..!!!


MAWAKILI wawili wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wanashikiliwa na kuhojiwa na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya yenye kifupisho cha lugha ya Kiingereza cha DCEA, kwa tuhuma za kuharibu kesi za 'unga' siku za nyuma.

Kukamatwa kwa Mawakili wa Serikali hao ni matokeo ya ahadi ya mapema mwezi uliopita ya Kamishana Mkuu wa DCEA, Rogers Sianga.

Akikabidhiwa majina ya watuhumiwa 97 wa biashara ya dawa za kulevya na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda Februari 13, Sianga alisema kuna majaji, mahakimu na Mawakili wa Serikali ambao walivuruga kesi zinazohusiana na dawa za kulevya kwa makusudi siku za nyuma.

Alisema kutokana na kuwapo kwa hali hiyo, DCEA ingepitia kesi zote za nyuma ambazo Serikali ilishindwa licha ya kuwa na vidhibiti, ili kuwabaini na kuwachukulia hatua, ikiwamo kwa kupeleka orodha kwa mamlaka husika.

Akizungumza na Nipashe jana iliyotaka kujua idadi ya watuhumiwa wanasheria hao na jinsi walivyohusika kupindisha kesi hizo, Sianga alisema:

“Hili jambo ni lazima ukae vizuri kwa kuweka ushahidi vizuri, (lakini) wanasheria wawili kutoka Ofisi ya Mwansheria Mkuu wa Serikali (tayari) tumeshawakamata.

"Hatua inayofuata ni kukamata mahakimu na majaji.

"Tunakwenda hatua kwa hatua kuhakikisha taratibu za kisheria zinafuatwa.

Kamishna Sianga ambaye aliiambia Nipashe kuwa alizungumza wakati akiwa safarini, aliahidi kutoa ufafanuzi zaidi wa hatua hiyo baadaye.

"Lakini kimsingi majina tunayo tayari na kuna mwanasheria atakayesimamia zoezi hilo anayejua namna ya kuchukua hatua kwenye suala hilo.”

Kamishna Sianga aliteuliwa Februari 12, na siku iliyofuata alikabidhiwa ripoti yeye majina ya watu 97 ambao ilidaiwa na Makonda kuwa wafanyabiashara, vigogo wa serikali ya awamu ya kwanza hadi ya tano, watoto vigogo na wananchi wengine.

Kamishna huyo alisema watapitia kesi zote za madawa ya kulevya zilizowahi kuamuliwa miaka ya nyuma, ili kuweka wazi zilizoharibiwa kwa makusudi.

Akitolea mfano wa kesi ambazo amedai zilivurugwa na mahakimu, alisema ni kesi iliyokuwa na ushahidi uliokuwa wazi kuwa mtuhumiwa amemeza dawa za kulevya, lakini hakimu akasema kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa na matatizo ya vidonda vya tumbo.

Aidha, Machi 6, wakati Sianga akikabidhiwa ripoti ya dawa za kulevya kidunia iliyoonyesha robo tatu ya waathirika ni wanawake na watoto, alisema DCEA inawahoji vigogo watano.

Tangu hapo, iligundulika, mtoto wa Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, ambaye ni Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete, ni mmoja kati ya watu waliohojiwa na mamlaka hiyo.

MSUKUMO MPYA

Vita dhidi ya dawa za kulevya nchini imepata msukumo mpya tangu Makonda ataje orodha ya watu 65 ambao alitaka waisaidie polisi kuhusiana na biashara ya madawa ya kulevya Februari 8.

Kabla ya kutaja orodha hiyo iliyokuwa na viongozi wa dini, wafanyabiashara na wanasiasa, Makonda alikuwa ametoa orodha ya Polisi 12 na wasanii kadhaa ambao walitakiwa pia kufika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa mahojiano.

Lakini harakati za kuwakamata watumiaji, wauzaji na watu wenye taarifa kuhusu biashara ya dawa za kulevya katika jiji la Dar es Salaam na nchini kwa ujumla zilipata msukumo mkubwa siku nne baadaye, baada ya Rais Magufuli kutaka zisiache mtu yeyote.

“Hakuna mtu maarufu, mwanasiasa, waziri au kiongozi yoyote au mtoto wa fulani, askari ambaye anajihusisha na dawa za kulenya aachwe, hata awe mke wangu Janeth... kamata wote weka ndani,” alisema Rais Magufuli.

Alisema biashara ya dawa za kulevya nchini imefikia katika hali mbaya na kwamba zinauzwa kama njugu nchini.

Alitaka vyombo vyote vya ulinzi vinavyoendelea kupambana na dawa za kulevya viendelee na mapambano.

Alisema biashara ya dawa za kulenya inapoteza nguvu kazi za Watanzania wengi haswa vijana, na kwamba vyombo vyote vya ulinzi vinapaswa kushirikiana ili kuwakamata hao.

Rais Magufuli aliwataka wahusika kuuwinda mtandao wote unaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

“Haiwezekani wauzaji wapo mtaani wanatanua tu, hawakamatwi," alisema Rais Magufuli.

"Kwa mfano kuna muuzaji mkubwa yupo mkoani Lindi, alishikwa na dawa za kulevya lakini sijasikia hata siku moja akitangulizwa Mahakamani.

"Ninajua kuna viongozi wanamtetea.”

Rais Magufuli alikuwa akimzungumzia mtu anayeaminika kuwa 'mzungu wa unga' aliyekuwa akitafutwa zaidi nchini na Marekani pia.

Ali Khatibu Haji (50), maarufu kwa jina la Shikuba, alikamtwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Machi, 2014 baada ya kuwindwa kwa miaka miwili kabla ya kuhamishiwa mkoani Lindi.

Anatuhumiwa kuwa kiongozi wa genge lenye makao yake Afrika Mashariki lakini likiwa na uhusiano wa kibiashara mpaka China, Brazil, Canada, Japan, Marekani na Uingereza.