SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 29 Machi 2017

T media news

Imefichuka... Hivi Hapa Vitu Vitano Vilivyokwamisha Bajeti ya Kwanza ya Serikali ya Rais Magufuli


WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amewasilisha kiwango na ukomo wa bajeti kuu ya serikali kwa mwaka 2017/18, akisema itakuwa Sh. trilion 31.6.

Aidha, waziri huyo amebainisha vikwazo vitano vilivyosababisha changamoto katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha ambayo ni ya kwanza kuidhinishwa chini ya uongozi wa Rais John Magufuli.

Akiwasilisha mapendekeza hayo ya serikali kuhusu mpango wa maendeleo ya taifa na kiwango cha ukomo wa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha, Dk. Mpango alibainisha changamoto tano zinazowakabili katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha ambayo ilikuwa Sh. trilioni 29.539.

Alisema bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo ni asilimia 40 ya bajeti yote ya serikali kwa mwaka huu wa fedha, ndiyo iliyoathirika zaidi kutokana na changamoto hizo.

Serikali ilipanga kutumia Sh. trilioni 11.82 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 8.702 zilikuwa za ndani na Sh. trilioni 3.117 ni fedha za nje.

Dk. Mpango alisema hadi kufikia Februari mwaka huu, fedha zilizokuwa zimetolewa ni Sh. trilioni 3.975 ikijumuisha fedha zilizotolewa kwa Halmashauri, sawa na asilimia 34 ya bajeti yote ya maendeleo.

"Kati ya kiasi hicho, fedha za ndani zilikuwa Sh. trilioni 3.103 na fedha za nje Sh. bilioni 871.8," alisema.

VIGINGI VITANO

Akifafanua kuhusu vikwazo vya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Waziri Mpango alisema mojawapo ya changamoto ni pamoja na sehemu ya fedha kuelekezwa katika kulipia madeni kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni kuchelewa kupatikana kwa misaada na mikopo kutokana na majadiliano na washirika wa maendeleo kuchukua muda mrefu.

Dk. Mpango alisema changamoto ya tatu ni kupanda kwa riba ya mikopo ya kibiashara katika soko la fedha kimataifa.

"Hata hivyo, ni vyema kutambua kuwa mwenendo huu wa kupungua kwa misaada na mikopo, haikuwa kwa Tanzania pekee. Nchi nyingine za Afrika zimekumbwa na hali hii hasa katika misaada ya maendeleo kama vile Zambia, Cote d’Ivoire, Bostwana na Algeria," alisema.

Mpango alitaja sababu nyingine ya kutotekelezwa kwa kiwango kikubwa kwa bajeti ya maendeleo na mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka huu wa fedha kuwa ni matayarisho hafifu ya miradi.

Dk. Mpango alitaja changamoto ya tano katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu kuwa ni mwamko mdogo wa kulipa kodi kwa kuzingatia matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD’s).

Aidha, alisema serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo, mojawapo ikiwa ni kuhakikisha fedha zinazopatikana zinaelekezwa kwenye miradi yenye tija na pia kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara ili kuvutia uwekezaji nchini.

MAPATO, MATUMIZI KUFIKIA FEBRUARI

Akizungumzia mwenendo wa mapato na matumizi ya serikali hadi kufikia Februari mwaka huu, Dk. Mpango alisema mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia Sh. trilioni 15.372, sawa na asilimia 79 ya lengo.

Alisema kati ya fedha hizo, mapato ya kodi yalifikia Sh. trilioni 9.306, sawa na asilimia 95 ya lengo la kukusanya Sh. trilioni 9.764, mapato yasiyo ya kodi yalifikia Sh. trilioni 1.305 sawa na asilimia 72.5 ya lengo la kukusanya Sh. trilioni 1.806.

Aliongeza kuwa mapato ya mamlaka za serikali za mitaa yalikuwa Sh. bilioni 310.6, sawa na asilimia 70 ya lengo la kukusanya Sh. bilioni 443.6; mikopo ya ndani ilifikia Sh. trilioni 3.506, sawa na asilimia 78 ya makadirio ya Sh. trilioni 4.479 na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ilikuwa Sh. trilioni 1.253, sawa na asilimia 40 ya lengo la Sh. trilioni 3.117.

MIKOPO KIBIASHARA YASHINDIKANA

Dk. Mpango alisema chanzo kingine ambacho kilitarajiwa kuipatia serikali fedha za utekelezaji wa bajeti ni mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara ambapo kwa mwaka huo ilipanga kukopa Sh.Trilioni 2.100 ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Hata hivyo, mtaalamu huyo wa uchumi alisema hadi kiufikia Februari mwaka huu, seriklai haikuweza kukopa katika chanzo hicho kutokana na hali ya soko la fedha la kimataifa kutokuwa nzuri.

Katika kipindi hicho, alisema riba ilipanda kutoka wastani wa asilimia sita hadi wastani wa asilimia tisa, jambo lililoilazimu serikali kuahirisha mchakato wa kukopa kutoka kwenye masoko hayo.

Aliongeza kuwa gharama za ukopaji katika masoko ya Ulaya imeanza kuimarika na kwamba tayari serikali imesaini mikataba mbalimbali kwa ajili ya kupata fedha.

UPATIKANAJI WA FEDHA

Waziri Mapngo alibainisha kuwa kipindi cha Julai 2016 hadi Februari mwaka huu, jumla ya Sh. trilioni 16.152 zilitolewa kwa wizara, idara zinazojitegemea, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa.

Kati ya hizo, Dk. Mpango alisema Sh. trilioni 12.177 zilizotolewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri Sh. bilioni 126.3.

Aidha, waziri huyo alisema Sh. trilioni 3.975 zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri Sh. bilioni 177.6.

Kuhusu fedha za matumizi ya kawaida zilizotolewa, Dk. Mpango alisema zinajumuisha Sh. trilioni 4.266 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa serikali, Sh. trilioni 6.135 kwa ajili ya mahitaji ya mfuko mkuu wa serikali na Sh. trilioni 1.775 za matumizi mengineyo.

VIPAUMBELE

Dk. Mpango alisema maeneo ya kipaumbele kwa mwaka ujao wa fedha ni miradi iliyobainishwa kuwa kielelezo na inatarajiwa kutoa matokeo makubwa kuendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na mpango wenyewe.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kati ambao mkandarasi wa kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki kwa kushirikiana na Mota-Engil Afrika ya Ureno wamesaini mkataba kwa kusanifu na kujenga awamu ya kwanza na ujenzi unatarajiwa kuanza mwaka huu.

Mingine ni ukamilishaji malipo ya ununuaji ndege tatu za serikali, mradi wa chuma Liganga, makaa ya mawe Mchuchuma, uanzishwaji wa kanda maalumu za kiuchumi ambazo ni Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Ruvuma na Mtwara.

Dk. Mpango alitja miradi mingine kuwa ni ya gesi asilia, shamba la kilimo na uzalishaji sukari Mkulazi.

Kadhalika, alisema serikali itaendelea kutekeleza miradi mingine ya kipaumbele ambayo ni ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa eneo la viwanda Tamco, Kiwanda cha General Tyre mkoani Arusha, mradi wa magadi Soda, kuimarisha mfumo wa taifa wa maendeleo ya wajasiriamali, uendelezaji wa viwanda vidogo na ujenzi wa ofisi za Sido.

Waziri huyo pia alisema kipaumbele kingine ni kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu, mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara, kuimarisha mitaji na kutumia benki za ndani za maendeleo TIB na TADB, na kuhamishia shughuli za serikali kuu makao makuu Dodoma ambapo tayari wizara zimeelekezwa kutenga fedha.

VIHATARISHI VYA BAJETI

Waziri huyo alisema vipo viashiria mbalimbali ambavyo vinaweza kuathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo -- vya ndani na nje ambavyo ni mtikisiko wa kiuchumi kikanda na kimataifa, majanga ya asili, athari za mabadiliko ya tabia nchi, mabadiliko ya kiteknolojia na ufinyu wa rasilimali fedha na watu.

Kutokana na hali hiyo, aliseman serikali itachukua hatua kupunguza utegemezi kwa kuwianisha mapato na matumizi, kuongeza mapato ya ndani na kuboresha mazingira ya kibiashara.

SERA YA MAPATO 2017/18

Dk. Mpango alisema kuwa katika mwaka ujao wa fedha, mapato ya ndani ya serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kupunguza nakisi ya bajeti.

Alitaja malengo ya mwaka 2017/18 kuwa ni kuongeza mapato ya ndani hadi kufikia asilimia 15.9 ya Pato la Taifa, kuongeza mapato ya kodi kufikia asilimia 14.1 ya Pato la Taifa, kupunguza nakisi ya bajeti kutoka asilimia 4.5 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17 hadi asilimia 3.8 mwaka 2017/18.

Alisema serikali imedhamiria kuimarisha ukusanyaji mapato ikiwa ni pamoja na kusimamia matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki, kupanua wigo wa walipakodi, kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija.

SURA YA BAJETI 2017/18

Dk. Mpango alisema katika bajeti ya 2017/18, serikali inatarajiwa kukusanya Sh. trilioni 31.6 ambazo zitatumika katika kipindi hicho, ambayo yatatokana na mapato ya halmashauri yanayotarajiwa kuwa Sh. trilioni 19.9 sawa na asilimia 63 ya bajeti yote.

Dk. Mpango alisema kati ya mapato hayo, mapato ya kodi ni Sh. trilioni 17.106, sawa asilimia 85.6 ya mapato ya ndani, huku mapato yasiyo ya kodi na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri yakiwa Sh. trilioni 2.1 na Sh. bilioni 687.3 kwa mtiririko huo.

"Ili kuhakikisha upatikanaji wa mapato hayo, serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa mapato na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato," alisema.

Waziri Mpango alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh. trilioni 3.9 (sawa na asilimia 12.6 ya bajeti yote), ikiwa misaada na mikopo hiyo ikijumuisha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, mifuko ya pamoja ya kisekta na ya kibajeti (GBS).

Dk. Mpango alisema serikali inatarajiwa kukopa Sh. trilioni 6.1 kutoka masoko ya ndani, lakini kati ya kiasi hicho Sh. trilioni 4.9 zitatumika kulipia hati fungani na dhamana za serikali zinazoiva (rollover) na Sh. trilioni 1.208 ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

“Ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu, serikali iinatarajiwa kukopa Sh. trilioni 1.5 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara," alisema.

MATUMIZI

Dk. Mpango alisema katika mwaka 2017/18, serikali inapanga kutumia Sh. trilioni 31.6 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo, kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 19.7 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikuijumuisha Sh. trilioni 7.2 za mishahara ya watumishi wa serikiali na taasisi huku Sh. trilioni 9.4 za kulipia deni la taifa.

Alisema fedha zilizotengwa katika bajeti ya maendeleo zimeongezeka kutoka Sh. trilioni 11,820 mwaka huu hadi Sh. trilioni 11.999 kwa mwaka ujao wa fedha, sawa na asilimia 38 ya bajeti yote.

Mwaka 2015/16, Bunge liliidhinisha bajeti ya serikali ya Sh. trilioni 22.5, bajeti ya mwaka 2014/15 ilikuwa Sh. trilioni 19.85 na ya mwaka 2013/14 ilikuwa Sh. trilioni 18.2.

Credit - Nipashe

*Imeandikwa na Augusta Njoji na Daniel Mkate (DODOMA), Sanula Athanas (DAR).