SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 29 Machi 2017

T media news

Aliyeunguzwa na Mumewe Amshukuru Rais Magufuli..!!!


RAIS Dk. John Magufuli, amepongezwa kwa moyo wake wa kujitoa na kuwajali wanyonge hasa wagonjwa wasiojiweza na wenye mahitaji ya gharama za matibabu.

Neema Wambura, maarufu kama ‘Mgonjwa wa Magufuli’ alisema hayo jana alipotembelewa na waandishi wa habari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alilazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kupata majeraha ya moto.

“Ninamshukuru sana Rais Magufuli kwa msaada wake katika matibabu yangu. Hivi sasa nina maendeleo makubwa, naweza kuzungumza, kula na hata kugeuza shingo yangu.

Nitamwombea Rais Magufuli mpaka siku naingia kaburini, Mungu ambariki,” alisema.

Akisimulia mkasa uliompata, Neema alisema alimwagiwa maji ya moto na mumewe baada ya kuchuma mahindi mawili shambani bila ya ruhusa yake.

Mumewe huyo alitoweka na ndugu zake walihofia kumchukua kwa kuogopa kudaiwa mahali iliyolipwa na mumewe kama taratibu za kumuoa.

“Hakuna ndugu yangu hata mmoja aliyejitokeza kunisaidia kipindi chote cha matibabu.

Walihofia kama ningefariki dunia ingempasa huyo ndugu kurudisha mahali ambayo mume wangu alitoa. Nilikuwa nasaidiwa na majirani tu, nilikata tamaa ya kuishi na nilikuwa nasubiri siku yangu ya kufa ifike,” alisema.

Neema pia aliwashukuru watumishi wa Muhimbili wodi ya Mwaisela wakiwamo wauguzi na madaktari kwa upendo na msaada mkubwa waliompatia tangu siku walimpokea mpaka sasa wakati anatarajia kurudi nyumbani.

Akielezea maendeleo ya afya ya Neema, Mkurugenzi wa Upasuaji wa MNH ambaye pia ni Daktari bingwa wa upasuaji, Dk. Ibrahimu Mkoma, alisema mgonjwa huyo alipokewa hospitalini hapo Julai 6, 2015 akitokea Musoma mkoa wa mara huku akiwa na majeraha ya mwaka mmoja toka aunguzwe.

Alisema mpaka sasa ameshafanyiwa oparesheni tatu kwa nyakati tofauti, zilizohusisha kutenganisha baadhi ya viungo kwa kuwa shingo, kifua na mkono wa kushoto vilishikana.

Pia alisema ilibidi kutoa ngozi ya sehemu ya mwili ili kufunika sehemu zile zilizoathirika zaidi.

“Ni katika kipindi hicho cha matibabu, Rais alimwona Neema na kuguswa na hali yake na kuamua kumsaidia mpaka hivi sasa mnavyomwona. Neema sasa amepona na ataweza kuihudumia familia yake vizuri,” aliongeza Dk. Mkoma.