SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 26 Machi 2017

T media news

Ushauri wa Samatta kwa wachezaji wanaokwenda kwenye majaribio halafu wanarudi

Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania Mbwana Samatta anaecheza soka la kulipwa Ubelgiji amewashauri wachezaji wa kibongo kutumia vizuri nafasi chache zinazopatikana za kwenda kufanya majaribio nje ya nchi kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa.

Samatta amesema, nafasi zinapotokea wanatakiwa kutumia hadi uwezo wao wa mwisho ili kulazimisha kutoka na pale inapotokea hawajachaguliwa, basi iwe imeshindikana kabisa na kila mtu ataona hivyo.

“Wanapopata nafasi za kutoka Tanzania kwenda kwenye timu nyingine wazitumie, kwa sababu tumeona wachezaji wengi wakitoka kwenda kwenye timu nyingine lakini wamekuwa wanarudi, inaonesha kwamba hawalazimishi kufanikiwa kutokana na nafasi zinazopatikana kwa kutumia vipaji vyao.”

“Muda mwingine inabidi umalize kile ulichonacho ili kuweza kupata nafasi, inapopatikana nafasi tuwe tunalazimisha isiwe rahisi tu mtu anaenda kwenye majaribio halafu anarudi. Inapotokea amerudi basi iwe imeshindikana kwa kiasi cha mwisho kabisa.”

“Na inapotokea imerudi nyumbani haimaanishi umefeli, unakuja kuanza tena upya sio lazima uende na ukafanikiwa moja kwa moja. Ukishindwa unakuja kujipanga kwa ajili ya nafasi nyingine, kwa hiyo mwisho wa siku nafasi inapopatikana walazimishe hadi mwisho, ikishindikana kila mtu ataona imeshindana.”

Mara kadhaa wachezaji wa bongo hususan wale wanaocheza ligi likuu Tanzania bara, wamekuwa wanapata nafasi za kwenda kufanya majaribio kwenye vilabu vya nje ya nchi kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa, lakini mwisho wa siku wanarudi nyumbani baada ya kushindwa kuvivutia vilabu hivyo.