SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 26 Machi 2017

T media news

Hatarii..Prof Lipumba Azidi Kumganda Maalim Seif,Adai ni Msaliti..!!!


Mwenyekiti wa CUF anayetambulia na Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amemlalamikia Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharrif Hamad kufungia akaunti zote za chama hicho za wilaya.

Akizungumza kwenye kikao cha baraza la uongozi linaloongozwa na upande wake, Profesa Lipumba amesema kutokana na uamuzi huo ruzuku ya chama kutoka serikalini wameikosa.

Mwanasiasa huyo amesema CUF ipo katika mtihani kwa sasa, hivyo uwapo wa Maalim katika kikao hicho ungesaidia kuiimarisha.

“Wajumbe nawashukuru kwa kuja ili kupata fursa ya kujenga chama. Chama chetu kipo ndani ya mtihani ambao kwa kweli chanzo chake ni katibu mkuu wetu kutoheshimu katiba yetu na kutoheshimu taratibu za kidemokrasia,” amelalamika Profesa Lipumba.

Amesema kuwa Maalim Seif alitakiwa kuhudhuria kikao hicho na alipewa taarifa lakini hakuweza kufika, hali iliyosababisha majukumu yake kusimamiwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), Magdalena Sakaya kama katiba yao inavyoelekeza.

 “Fedha zimekwama kwenye mabenki hasa NMB kwa sababu akaunti za wilaya zinafunguliwa na kamati za utendaji za wilaya, hazifunguliwi na makao makuu, lakini wenzetu wametumia mitandao ya wapambe wao kutoa shinikizo zifungwe,” amesema.

Akijibu tuhuma hizo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Mazrui amesema kuwa hatua ya kufunga akaunti za benki imelenga kulinda fedha ya chama ili zisitumiwe vibaya na upande wa Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba yupo kwenye mgogoro na CUF baada ya kuandika barua ya kujiuzulu na baadaye kuifuta, lakini mkutano mkuu ulikubali kujiuzulu kwake na kuteua kamati ya uongozi chini ya Julius Mtatiro.

Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa bado anamtambua kwa madai kuwa hakutaarifiwa kuhusu uamuzi huo na kwamba, baadhi ya taratibu hazikufuatwa, msimamo ambao CUF chini ya Maalim Seif imeukataa.