Taarifa ya siku ya kwanza ya ziara ya mahsusi ya mazingira ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba kutembelea mikoa ya Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Singida yenye lengo la kutambua changamoto za kimazingira na kuweka mikakati sahihi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuweka mahusiano bora zaidi katika utunzaji wa Mazingira kati ya Serikali Kuu, Serikali za Mtaa, watu binafsi na taasisi za kimazingira.
Waziri Makamba ameanza ziara mahsusi ya kimazingira katika mikoa 6 inayolenga kutambua, kufahamu na kupatia majawabu ya changamoto za kimazingira zinazoikabili mikoa hiyo. Waziri Makamba ameanza ziara hiyo mkoani Pwani kwa kutembelea na kukagua changamoto za kimazingira katika Halmashauri za Bagamoyo na Chalinze huku akitarajiwa kuendelea katika mkoa wa Tanga
Waziri Makamba anafanya ziara hii mahsusi ikiwa ni mwendelezo wa kufahamu na kuchukua hatua stahiki dhidi ya changamoto mbalimbali za kimazingira baada ya ziara ya kwanza aliyoifanya katika mikoa 10 mwishoni mwa mwaka jana. Katika Wilaya ya Bagamoyo Waziri ametembelea na kukagua eneo la Mto Mpiji unaotenganisha mkoa wa Dar es Salaam na Pwani eneo la Kata ya Mapinga kitongoji cha Kibosha ambapo amekagua shughuli za utunzaji mto huo ambao unakabiliwa na changamoto kubwa ya uchimbaji wa mchanga kwaajili ya shughuli za kibinadamu ikiwemo mahitaji ya ujenzi.
Waziri Makamba bada ya ukaguzi huo ameiagiza Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya doria, kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote wanaohusika na kuchimba mchanga katika mto huo kinyume na taratibu kwani uchimbaji huo unaharibu kwa kiasi kikubwa hali ya mto. Vilevile Waziri Makamba ameagiza ndani ya wiki mbili kuanzia tarehe 20 Machi 2017 mamlaka husika zihakikishe zinasimamia uwekwaji wa alama za mipaka (beacon) ndani ya mita 60 za mto na pia kuwataka wale wote wanaofanya shughuli za kibinadamu ndani ya eneo la mto huo kama kilimo kuacha mara moja na wale waliofanya makazi wahame mara moja huku akiwapa mwezi mmoja kufanya hivyo baada ya kuombwa na Balozi wa Kibosha, Ndugu Julius Mapunda aliyeomba wananchi wake kupewa angalau mwezi mmoja ili kujipanga kuhama tofauti na wiki mbili zilizokuwa zimeagizwa na serikali.
Waziri pia kwa niaba ya Serikali ameahidi Halmashauri ya Bagamoyo kwa ushirikiano na wananchi kushughulikia eneo la karibu na mto lenye korongo linalofuata makazi ya watu hali inayosababishwa mmonyoko na kuhatarisha maisha ya watu.
Waziri Makamba alifika pia katika Halmashauri ya Chalinze ambapo alitembelea Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Chalinze(CHALIWASA) ambapo pamoja na kutembelea na kukagua la mto Wami vilevile alipokea taarifa ya fupi ya CHALIWASA pamoja na changamoto za uchafuzi wa mto Wami.
Waziri Makamba amesikitishwa na suala la mradi wa maji Wami kufanya kazi kwa asilimi ndogo sana na hata wakati mwingine kufikia asilimia 8 tu kwani uwezo wa mradi wakati wa ufunguzi wa mradi ulikuwa ni lita Milion 7.2 kwa siku lakini ufanisi hivi sasa umepungua hadi kufikia lita Milioni 4.8 kwa siku sababu kubwa ikiwa ni uharibifu wa mazingira unaofanywa hasa katika vyanzo vya maji vinavyomwaga maji yake katika mto huo hivyo kupelekea mto kuwa na mchafuko/tope jingo hasa nyakati za mvua
“Tatizo kubwa la kijamii la kwanza ni upatikanaji wa maji, kuna jitihada kubwa sana zinafanywa na serikali ya awamu ya tano ambayo imedhamiria kuwekeza kwenye miundombinu ya maji,lakini kuwekeza ni jambo moja na utunzaji wa vyanzo hivyo ni jambo jingine hivyo uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji ni ya muhimu zaidi”. Aliainisha Waziri Makamba mwenye dhamana ya kusimamia mazingira nchini.
Ili kunusuru hali mbaya inayoendelea hivi sasa Waziri ameahidi kusimamia ofisi yake kuandaa mkutano wa wadau wakubwa wa mito na vijito pamoja na wanufaika wa maji ya Mto Wami ambao utaunda mkakati wa pamoja ikiwa ni pamoja na kupeana kazi katika kuokoa mradi huo ambao kwa sasa ufanisi wake umeshuka. Amesisitiza kuwa hautakuwa mkutano wa maneno bali mkutano wa kazi na kutafuta majawabu ya kuona njia bora na sahihi zaidii za kuzuia shughuli za kibinadamu katika maeneo ya mto huo hasa kilimo ufugaji na uchimbaji haramu wa madini kandokando ya vidaka (catchment) za mto huo.
Waziri Makamba pia amefanikiwa kufika katika hifadhi ya Taifa ya msitu wa Uzigua wenye ukubwa wa takribani ekati 24436 na kushuhudia uvamizi wa hali ya juu na uharibifu wa eneo la hifadhi ya msitu huo unaotokana na shughuli za kibinadamu hasa kilimo, ufugaji na ukataji miti bila vibali kwaajili ya uchomaji make. Hifadhi hiyo ya Taifa ya Msitu ambayo ipo katika wilaya tatu za Bagamoyo kwa 96 huku asilimia 4 zikiwa katika wilaya za Handeni na Kilindi una vyanzo vingi vya maji vinavyomwaga maji yake katika Mto Wami ambavyo viko hatarini kukauka kutokana na uharibifu unaoendelea
Ili kushughulikia moja kwa moja hali ya uharibifu katika Msitu huo, Waziri Makamba amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Kibindu ambao kwa kiasi kikubwa wanafanya shughuli za kilimo katika eneo la hifadhi. Waziri Makamba amewataka wananchi hao kufuata taratibu na njia sahihi zilizowekwa kisheria katika kuomba kupewa ardhi ya ziada ambao wataainisha mambo ya msingi ikiwemo ukubwa wa ardhi wanaohitaji, matumizi ya sasa ya sasa ya ardhi pamoja na mpango wa matumizi bora ya ardhi wanayoiomba huku Waziri akiwaweka wazi wananchi na viongozi waliohudhuria katika mkutano kuwa maombi lazima yaanzie katika mkutano rasmi wa wanakijiji utakaothibitisha kuwa ni wananchi ndio wenye mahitaji lakini pia akiahidi kuhakikisha mamlaka husika zinasimamia mchakato huo ipasavyo.
Waziri Makamba amewaweka wazi wananchi hao kuwa wanapaswa kuacha kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ambayo ni ya hifadhi ya msitu kwani kuendelea kufanya hivyo na kuvunja sheria za nchi, vilevile ameziagiza mamlaka husika kufanya doria mpya kuwaondoa wavamizi wanaofanya shughuli zao katika maeneo ya hifadhi ya msitu kinyume na taratibu wakiwemo wafugaji waliovamia maeneo tengwa.
Waziri Makamba anaendelea na ziara yake hii leo ambapo anatarajiwa kufika katika mkoa wa Tanga