Kocha maarufu nchini ‘Julio’ ametoa ushauri kwa klabu ya Yanga baada ya ratiba ya kombe la shirikisho Afrika kutoka na kuwakutanisha mabingwa watetezi wa taji la VPL na AC Alger.
Julio amesema, Yanga wanatakiwa kujiandaa vizuri kwa ajili ya kuwakabili wapinzani wao ambao ni waarabu kutoka Algeria.
“Yanga wanatakiwa wajiandae vizuri kwa ajili ya mechi dhidi ya waarabu kwa sababu mara nyingi wamekua wakitolewa na timu za kiarabu, wanatakiwa kuwaandaa pia wachezaji wao kisaikolojia.”
Julio ambaye aliwahi kucheza Simba na badae kuwa kocha wa timu hiyo, amesema hawaombei mabaya Yanga kwa sababu wanaiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo ya bara la Afrika.
Kuhusu Azam kutupwa nje ya mashindano ya kombe shirikisho, Julio amesema: “Azam walijiamini sana baada ya kupata ushindi wa goli 1-0 dhidi ya wapinzani wao Mbabane Swallows.”
“Azam walijua mechi imeishia Azam Complex hivyo wanakwenda kumaliza kazi ugenini, lakini walichokutana nacho Swazland kiliwashangaza wote baada ya kuchapwa 3-0. Vurugu ambazo walifanyiwa nje ya uwanja hazikua na athari kubwa ndani ya uwanja kwa hiyo isiwe kama kisingizio.”
“Azam walizidiwa kuanzia mechi ya kwanza Azam Complex na naamini kwa matokeo ya mechi yao ya marudiano walizidiwa pia hata ugenini.”